Pages

Thursday, December 6, 2012

SHIRIKISHO LA SOKA NCHINI LATAKA WACHEZAJI WA CONGO BRAZAVILLE WAPIMWE UPYA

Wachezaji wa U-17 wa Congo Brazaville waliocheza na Serengeti boys
Serengeti boys


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewasilisha barua ya malalamiko yake dhidi ya matumizi ya wachezaji wenye umri mkubwa na unyanyasaji uliofanyuwa kwa maofisa wa timu ya taifa ya vijana walio na umri chini ya miaka 17 wa Serengeti Boys wakati wa mechi ya marudiano ya michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Vijana dhidi ya Congo.

Serengteti Boys iliondolewa kwenye mashindano hayo kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya kwanza iliyofanyika Novemba 18, 2012 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar Es salaam na baadaye kukubali kipigo cha mabao 2-0 kwenye mechi ya marudiano jijini Brazaville Jumapili iliyopita.

Hata hivyo, mechi hizo mbili zilizingirwa na matukio tata, hasa kuhusu umri wa wachezaji wa Congo ambao kimaumbile walionekana kuwa ni umri mkubwa zaidi na kusababisha TFF kuwasiliana na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) kuhusu njia zinazowezekana kupata uthibitisho wa umri wa wachezaji hao, lakini ilishindikana na ndipo TFF ilipocheza mechi hiyo ikiwa na imeweka pingamizi.
Katika barua iliyotumwa CAF jana, TFF imerejea barua ya pingamizi aliyokabidhiwa kamisaa wa mechi ya kwanza jijini Dar Es salaam, Bw. Chayu Kabalamula na malalamiko yaliyowasilishwa kwa kamisaa wa mechi ya marudiano kuhusu vurugu walizofanyiwa maofisa wa timu.

Katika barua hiyo, TFF imeomba CAF iagize kuwa wachezaji wote wa Congo waliocheza mechi hizo mbili wapimwe tena kwa kutumia kipimo cha M.R.I na gharama za zoezi hilo zilipiwe na TFF; na pili Shirikisho limeomba kuwa CAF ikubali kuipa Tanzania wiki tatu za kukusanya ushahidi na kuuwasilisha Cairo kwa ajili ya maamuzi.

Kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, nchi shiriki zinatakiwa kuwapima wachezaji wake kwa kutumia kipimo cha M.R.I ambacho kinaweza kutambua umri wa vijana walio chini ya miaka 17 na kwamba matokeo yake yanatumwa CAF, ambayo itahifadhi matokeo hayo hadi hapo kutakapotokea pingamizi na ndipo itafanyia kazi kwsa kutoa matokeo ya vipimo hivyo.

“Ni matumaini yetu kuwa suala letu litafanyiwa kazi na kutolwewa ufumbuzi ili kulinda soka la vijana barani Afrika dhidi ya vitendo vilivyokomaa vya udanganyifu wa umri,” alisema katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jana, kocha Jacob Michelsen alisema alishangaa kuona wachezaji wenye umri mkubwa zaidi wakichezeshwa kwenye mechi ya marudiano, lakini akaisifu TFF kuwa inafuata njia sahihi ya maendeleo na haina budi kuendelea na programu yake ya soka la vijana.
"Najivunia vijana wangu kwa kuwa walijituma kwa muda wote pamoja na kwamba wenyeji waliongeza wachezaji wenye umri mkubwa zaidi kuliko waliokuja huku," alisema kocha huyo kutoka Denmark.

"Kitu cha msingi ni kufuata njia sahihi ya kuendeleza soka na natumaini TFF iko kwenye njia sahihi na itaendelea na programu yake ya vijana. Hakuna njia ya mkato kama mnataka maendeleo. Ni lazima tufuate njia sahihi na matunda yake tutayaona baadaye.
"Kila mara nasema mambo (ya vijana) huchukua muda mrefu (Things Take Time) na hivyo hatuna budi kuwa wavumilivu.
"Wenzetu walitumia njia za ajabu na hata hiyo penati ya bao la kwanza haikuwa faulo. Ilitokea nje kabisa ya eneo la penati. Refa alimuangalia kibendera akaona ametulia, akamuangalia beki mchezaji akamuona amesimama, mara akaangalia juu na kupuliza filimbi kuonyesha kuwa ni penati."

Naye kocha msaidizi, Jamhuri Kihwelo alishindwa kujizuia na kujikuta akibubujika machozi wakati alipoelezea jinsi alivyoshambuliwa na askari kabla ya mchezo huo.

No comments:

Post a Comment