Pages
▼
Thursday, December 6, 2012
KOZI YA LESENI C KUFANYIKA ARUSHA
Kituo cha Kukuza Vipaji cha Rolling Stone kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kimeandaa kozi ya leseni C ya walimu wa mpira wa miguu itakayofanyika kuanzia Desemba 10, 2012 hadi Desemba 23, 2012 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
Kozi hiyo itahusisha makocha walio na Cheti cha Kumaliza Elimu ya Sekondari au wale waliohitimu kozi ya ualimu wa mpira wa miguu ya ngazi ya kati (intermediate).
Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni alisema kuwa washiriki wa kozi hiyo wanatakiwa kuwa wamewasili Arusha ifikapo Desemba 9, 2012 na wanatakiwa kwenda na vyeti vyao halisi vya elimu. Alisema tayari Rolling Stone wameshasajili walimu 25 ambao watashiriki kozi hiyo na hivyo kuwataka watu wengine wanye sifa kutoka mkoa wa Arusha na mikoa mingine kujitokeza kushiriki mafunzo hayo muhimu.
Kayuni alisema kuwa kadri taifa litakavyozalisha walimu wengi, ndivyo taifa litakavyokuwa na uwezo wa kuandaa watoto na vijana wengi katika misingi sahihi ya mpira wa miguu na hivyo kuwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri.
Kozi hiyo itaendeshwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Kayuni kwa kushirikiana na mkufunzi kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF), Bw. Dominic Niyonzima kutoka Rwanda.
Kwa mujibu wa Rolling Stone, kila mshiriki atajigharimia nauli ya kwenda Arusha na atatakiwa kwenda na ada ya fedha zinazolingana na
Dola 100 za Kimarekani (dola moja ni sawa na Sh1,580 za Tanzania).
No comments:
Post a Comment