Pages

Friday, December 7, 2012

OKWI ASAINI MKATABA WA MIAKA MIWILI NA SIMBA KAMPALA JANA USIKU

Emanuel Okwi akiwa na Felex Sunzu

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, anayechezea Simba Emmanuel Okwi ameongeza mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea timu hiyo ya Dar es Salaam, baada ya kusaini jana usiku katika hoteli ya Sheraton mjini Kampala.

Okwi alisaini mkataba huo mbele ya Mwenyekiti wa Simba SC, Ismail Aden Rage ambaye alikuwa ameongozana na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe.

Baada ya kusaini, Okwi alisema; “Nimefurahi kuongeza mkataba na klabu yangu na ninaahidi kuendelea kuitumikia kwa nguvu zangu zote.”

Kwa upande wake, Hans Poppe alisema kwamba anaamini kusaini na Okwi sasa kutawafanya mashabiki wa Simba kutulia na kuwakata vilimilimi wapinzani wao, ambao walikuwa wanamuwania mchezaji huyo.

“Sisi tunajua yote yaliyokuwa yakiendelea kwenye Challenge, tunajua wapinzani wetu walimfuata Okwi huku, lakini huyu mchezaji ana mapenzi yeye mwenyewe na Simba SC,”alisema Hans Poppe.

Okwi aliyezaliwa Desemba 25, mwaka 1992 mjini Kampala, alisajiliwa na Simba SC mwaka 2009 akitokea SC Villa ya Uganda.

Tangu msimu uliopita, Okwi amekuwa akihusishwa na mpango wa kuhamia Yanga au Azam na akiwa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA, ziliibuka habari za klabu hizo kumfuata kumsainisha mjini hapa.

Okwi jana alifunga bao moja kati ya matatu ya Uganda kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa, yaliyozima ndoto za Tanzania Bara kurejea nyumbani na Kombe la Challenge.

No comments:

Post a Comment