Pages
▼
Monday, December 24, 2012
IDDI MTINGOJA AUKWAA UENYEKITI WA KAMATI YA RUFAA YA UCHAGUZI WA TFF
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemteua Idd Mtiginjola kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF iliyoundwa kutokana na marekebisho ya Katiba yaliyofanyika hivi karibuni.
Mtiginjola ambaye ni Wakili wa kujitegemea ataongoza kamati hiyo yenye wajumbe watano ambayo sasa itakuwa chombo cha mwisho kusikiliza rufani zinazotokana na uchaguzi wa TFF, na wanachama wa TFF ambao hawatakubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Kabla ya uteuzi huo, Mtiginjola alikuwa mjumbe wa Kamati ya Nidhamu ya TFF inayoongozwa na Kamishna wa Polisi (CP) mstaafu Alfred Tibaigana. Nafasi yake katika kamati hiyo na ile ya mjumbe mwingine Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Shabani Semlangwa aliyefariki dunia Julai mwaka huu zitajazwa hivi karibuni.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF ambayo vinara wake (Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti) wanatakiwa kitaaluma kuwa wanasheria ni Francis Kabwe. Kabwe ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Wajumbe wengine walioteuliwa na Kamati ya Utendaji ya TFF katika kikao chake cha jana (Desemba 23 mwaka huu) ni Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Mohamed Mpinga ambaye pia kitaaluma ni Mwanasheria.
Wengine ni mshambuliaji wa zamani wa timu ya Reli Morogoro, Profesa Madundo Mtambo ambaye kwa sasa ni Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo mjini Morogoro, na mdau wa soka Murtaza Mangungu ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini.
No comments:
Post a Comment