Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Friday, November 16, 2012

UJIO WA PELE TANZANIA UZAE MATUNDA



.
“KIPAJI pekee hakiwezi kukufikisha kwenye mafanikio ila kujituma ndio kutakufanya ufanikiwe”, haya ni maneno aliyosema mwanasoka bora wa zamani Afrika, Abeid Ayew Pele ambaye pia ni Balozi wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) alipotembelea Tanzania hivi karibuni.
Pele ambaye alikuwa mshambuliaji  wa zamani wa kimataifa wa timu ya taifa la Ghana na klabu ya Olympique Marseille ya Ufaransa, aliwaambia wachezaji chipukizi wa Tanzania kwamba, hakuna njia ya mkato katika kutafuta mafanikio na kuwataka kufanya jitihada ili watimize ndoto zao, ikiwa ni pamoja na Serengeti Boys kuhakikisha inafuzu kucheza fainali za Afrika mwakani.

Pele, ambaye aliiongoza Marseille kutwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 1992 akifunga moja ya mabao dhidi ya AC Milan ya Italia, aliwaambia wachezaji chipukizi wakati alipotembelea kituo cha mafunzo kilicho chini ya Shirikisho la Soka Nchini cha Karume, na  kushuhudia programu ya mazoezi ya vijana wadogo inayofanyika kila mwishoni mwa wiki, ambako watoto wa kuanzia umri wa miaka minne hadi 17 hufundishwa mbinu za kucheza soka.
"Katika kufikia mafanikio hakuna njia ya mkato," alisema Pele ambaye alifanya ziara ya siku tatu nchini ambayo ilikuwa imeandaliwa na  Shirikisho la Kimataifa la Soka  Ulimwenguni (FIFA) kuangalia shughuli mbalimbali za maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
Hakuna ambaye atabisha juu ya kauli ya Pele kwani tunaona wachezaji wenye vipaji vikubwa duniani wakifanya jitihada kubwa ili waweze kucheza kwa kiwango cha juu kwani bila ya kufanya juhudi, kujituma na kudhamiria hawawezi kufanikiwa.
Wachezaji  wetu waliobahatika kuonana na Pele basi iwe chachu kwao ya kufikia mafanikio kama yake isiwe ilikuwa ni kupiga picha naye tu ikaishia hapo, bali watumie falsafa yake ya kuwa  kipaji vikubwa haviwezi kuleta mafanikio bali wafanye jitihada. Jitihada inayotakiwa hapa ni kufanya mazoezi kwa bidii tena kwa muda mrefu na kusikiliza makocha maana nidhamu pia hujenga na ikachangia mafanikio.
Mfano mzuri ambao wachezaji wa Tanzania wanaweza kujifunza juu ya kujituma na kufanya mazoezi muda mrefu ni Nonda Shaban raia ya Congo ambaye aliwahi kuichezea Yanga ya Dar es Salaam, Nonda wakati kocha anapanga program yake inaanza saa kumi jioni yeye saa nane mchana anakuwa uwanja akifanya mazoezi lakini kocha akifika anaendelea na programu yake na ndio maana aliweza kupata mafanikio ambayo yamemwezesha kucheza nje ya nchi.
Pele baada ya kuonana na wachezaji Karume na timu ya Taifa ya vijana waliochini ya miaka 17 “Serengeti boys” alitembelea kituo cha soka cha Azam kilichopo Chamazi ambapo pia ni makao makuu ya klabu ya Azam, maarufu kama  Azam Complex, jijini Dar es Salaam.
Akiwa Azam kwanza kabisa kabla hajasaini kitabu cha wageni alifanyiwa surprise ya kuimbiwa happy birthday na kukabidhiwa keki kubwa iliyopambwa uwanja wa soka ambapo siku hiyo alitimiza miaka 48.
Akiwa  Chamazi alijionea mambo mbalimbali ikiwemo mradi wa maendeleo ya soka ya vijana “ Academy” aliusifia sana na kusema utaleta matunda makubwa Tanzania baadaye, pia alitumia fursa hiyo kuelezea namna alivyoiona ligi kuu ya Tanzania kwani jana yake alihudhuria  Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo Yanga na Azam.
Pel>Pele ambayo pia anamiliki shule ya soka, alisema  Azam miaka kadhaa ijayo itakuwa klabu kubwa sawa na za Uingereza kutokana na uwekezaji wake mzuri. Pia alisema akademi ya Azam ni nzuri na bora kuliko hata akademi yake.
 “Kwetu kuna shule za soka nyingi, lakini nyingi ni za wawekezaji wa nje (klabu za Ulaya), lakini hii ya Azam ni nzuri kuliko shule yangu ambayo ni ndogo tu, haifikii hii kwa ubora, nami nina ndoto za kuwa na akademi kubwa kama hii, na nimejifunza mengi kutoka kwa Azam,”alisema Pele.
Pia Pele aliishauri Azam na vilabu vya Tanzania kuachana na desturi ya kuchukua wachezaji wa nje ya nchi, kwani kama wataitumia vizuri fedha wanazonunulia wachezaji wakawekeza  kusaka vipaji zaidi nchi mzima watapata wachezaji bora.
“Nawaahidi tutakuwa tunabadilishana uzoefu na  kama una akademi nzuri kama hii hakuna sasabu ya  kuchukua mchezaji kutoka Ghana, hii nchi yenu ina watu zaidi ya Milioni 40, mnaweza kutengeneza wachezaji wengi wazuri na nyinyi mkauza Ulaya,”alisema  Pele.
Akizungumzia Ligi Kuu ya Tanzania baada ya kuona mechi ya Yanga na Azam, Pele alisema ina ubora sawa na ligi nyingine kubwa Afrika na akasema sasa kinachotakiwa ni kuongeza maboresho pia wachezaji kulingana na alivyoona mchezo alioshuhudia wa Azam na Yanga alisema kwamba wana uwezo sawa na wachezaji wengi duniani  ili watimize ndoto za kucheza Ulaya, wanatakiwa kuongeza juhudi

"Soka barani Afrika lina mazingira yanayofanana, hakuna mtoto wa waziri, mwanasheria au wa mfanyakazi wa benki ambaye anacheza soka. Soka inachezwa na watoto wanaotoka kwenye familia ambazo hazina maisha mazuri hivyo wana nafasi sawa na wengine wote. Mnachotakiwa kufanya ni kujituma, kudhamiria na kufanya jitihada ili mfungue milango ya mafanikio” , alisema Pele, ambaye watoto wake wawili wanaichezea Marseille.
Pia aliwataka wachezaji wa timu ya Taifa ya Vijana walio na umri china ya miaka 17 kufanya kila wawezalo ili wafuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika nchini Morocco, Machi  mwakani. "Mkifuzu mtakuwa mmefungua milango ya mafanikio ya maisha yenu", alisema gwiji huyo ambaye anaiwakilisha FIFA katika kukagua na kufuatilia  programu mbalimbali za maendeleo ya soka nchini Tanzania.
“Nilivyowaangalia naona mna  uwezo wa kuwaondoa wapinzani wenu  DRC na nitafuatilia mechi yenu. Mkifuzu tutakuwa wote na nitawaunga mkono”, aliwaambia Serengeti boys.  Pele ambaye kwa sasa anamiliki shule ya mpira wa miguu (academi) alikuwa ameambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya soka wa FIFA kwa nchini za Kusini mwa Afrika, Ashford Mamelodi na Emmanuel Maradas mjumbe wa Idara ya Mawasiano ya FIFA ,  walikaa nchini kwa siku tatu ambazo walizitumia kupata taarifa za shughuli mbalimbali za maendeleo, zikiwemo za soka la watoto (grassroots), soka la vijana, soka la wanawake na miradi ya viwanja vinavyokarabatiwa na FIFA kama ule wa Nyamagana Mwanza na Zanzibar.
Shirikisho la Soka nchini kupitia idara ya ufundi linatakiwa kuwekeza zaidi kwenye shule za  soka ili kuwapa fursa zaidi vijana wadogo kuonyesha vipaji vyao ili viweze kuendelezwa. Nasema hivi kwa sababu TFF wana uwezo wa kuamuru kila chama cha soka cha mkoa nchini kiwe na darasa la shule za soka kila jumamosi na jumapili na kwa sababu karibu mikoa yote ina viwanja na makocha wataweza kufanya hivyo. Pamoja yote pia ligi za vijana viwepo siyo mpaka Copa cocacola tu ambayo pia vile vipaji vinavyopatika vinapotea  tu kwa sababu hakuna mahali maalumu pa kuwaweka ili kuendeleza vipaji hivyo.
Pia wasisitize timu zinazocheza ligi kuu zianzishe shule za soka ili kupunguza fedha wanazotumia kununua wachezaji wa kigeni wawekeze kwenye shule za soka. Kwa kufanya hivyo wanaweza kuuza wachezaji nje baadaye na watakuwa na vipaji na wachezaji wanaoujua mpira kisawasawa.
Wachezaji wa kitanzania ambao mnajua mna kipaji cha kucheza soka mjitume na nidhamu pia iwe ndio ngao yenu  ili mfike kwenye mafanikio muweze kujisaidia wenyewe, familia zenu na nchi yetu. Najua kwa sasa upo mfano mzuri wa kuiga ambao ni Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu vijana wadogo wanaochezea TP Mazembe ambao utajiri unawanukia kabla ya kufikisha miaka 20. Mlikuwa mnawaona wakicheza mpira wakiwa uwanja wa Karume wakati kuna ile shule ambayo Shirikisho la Soka nchini lilikuwa na mkataba na Bolton Wonderus ya Uingereza mkataba ambao hata hivyo ulivunjika na kila mchezaji kurudi kwenye timu zao za awali na wengine kusajiliwa na Yanga, Mtibwa, African Lyon na Simba. Baadhi ya wachezaji waliotoka kwenye shule hiyo ambayo makao yake makuu yalikuwa kwenye hostel zinazomilikiwa na TFF zilizopo Karume ni Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu, Simon Msuva,  Issa Rashid “baba ubaya”, Omega Seme, Jamal Mroki, Barwany Khomein, Jerome Lambele, Leonard Muyingwa na wengine wengi.

Tuache kulalamika tujitume wenyewe mafanikio yatafuata nyuma ili ziara ya Pele isiwe alikuja tupige naye picha za kutundika ukutani au kuweka kwenye albamu tu bali iwe ni kumbukumbu ya kutusukuma tufikie mafanikio kama yake na pengine zaidi yake. Natoa hoja.

No comments:

Post a Comment