Pages

Thursday, November 1, 2012

MECHI YALALA KISA MVUA, SASA KUMALIZIWA LEO

MVUA kubwa iliyonyesha mjini Mbeya imesababisha mchezo wa ligi daraja la kwanza kati ya Mbeya City na Mlale kushindwa kuendelea likiwa limemalizika kipindi cha kwanza tu.

Akizungumza na LENZI YA MICHEZO kwa njia ya simu toka Mbeya msimamizi wa kituo hicho Seleman Haroub alisema kuwa mchezo huo ulishindikana kuendelea kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha uwanja wa kujaa maji.

"Mchezo ulishindikana kuendelea kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha uwanja kujaa maji, zilikuwa zimebaki dakika 45", alisema Haroub.

Mchezo huu ambao ni wa kundi A mpaka unasimama Mbeya City walikuwa wanaongoza kwa mabao mawili yaliyofungwa na Fidelis Castory dakika ya 14 na Hassan Mwasapili dakika ya 34.

Kutokana na mabadiliko ya kanuni za ligi mchezo huu utachezwa au utaendelezwa kuchezwa dakika zilizobaki na matokeo yanaendelea yale ya mchezo uliposimama.

Kwenye uwanja wa Mandela mkoa wa Rukwa wenyeji Small Kids waliitandika bila huruma Mkamba mabao 3-0 kupitia kwa Salum Mdemi dakika ya 25 na Adam Karisti alifunga mawili dakika ya 33 na 88.

Mjini Iringa Polisi Iringa na Kurugenzi zote za Iringa walitoshana nguvu kwa kutoka sare ya 1-1

Mchezo wa Majimaji ya Ruvuma na Burkinafasso ya Mororgoro uliahirishwa  kutoka na Burkinafasso kuchelewa kufika Ruvuma.

Kwenye michezo ya kundi C timu ya Kanembwa ya Kigoma iliwabugiza wachimba dhahabu wa Shinyanga Mwadui FC mabao 3-2 kwenye mchezo uliochezwa uwanja wa Lake Tanganyika.

Mchezo huo ambao Kanembwa walioutawala sana mpaka kuwatia presha wapinzani mpaka wakajifunga ulikuwa burudani kwa wakazi wa Lake Tanganyika na Vitongoji vyao.

Magoli ya Kanembwa yalifungwa na Baruan Akilimali dakika ya 20 na 87 na la tatu alijifunga Nasibu Malila  dakika ya 73 na Mwadui walijipatia mabao yao kupitia kwa Chuku Chika dakika ya 35 na Mtitu Moses dakika ya 85.

Uwanja wa Jamhuri wenyeji Polisi Dodoma waliifunga Pamba ya Mwanza mabao 2-1.

Kwenye uwanja wa Karume mkoani Mara Polisi Mara na Rhino ya Tabora walitoka suluhu ya 0-0.

Mchezo kati ya Moran na Polisi Tabora hakuchezwa kutokana na Moran kuchelewa kufika kwani mchezo uliopita walicheza Kigoma na Kanembwa Octoba 27.

No comments:

Post a Comment