Pages

Sunday, November 25, 2012

KILIMANJARO STARS KUIVAA SUDAN BILA SAMMATA NA ULIMWENGU

Wachezaji wa Kilimanjaro stars wakifanya mazoezi kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Makere nchini Uganda jana
Mwinyi Kazimoto na Mrisho Ngassa wakiwa kwenye  mazoezi ya Taifa Stars  uwanja wa Karume, jijini Dar es salaam

TIMU ya Taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), leo inatupa karata yake ya kwanza ya michuano ya Chalenji dhidi ya Sudan ya Khartoum kwenye Uwanja wa Nambole, jijini Kampala.

Stars na Sudan ziko Kundi B, na mechi yao inatarajiwa kuanza saa 12 jioni, lakini awali kutachezwa mechi kati ya Burundi na Somalia, saa tisa mchana.
Katika mchezo huo, Stars inahitaji zaidi kuibuka na ushindi ambao utaiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele.

Stars italazimika kupigana kiume kuishinda Sudan, ambayo rekodi za viwango vya  ubora vya Shirikisho la Soka la Dunia (Fifa) mwezi huu, vinaonyesha Sudan ikiwa nafasi ya 102 na Tanzania nafasi ya 132.

Kwa upande mwingine, kocha wa Stars, Kim Poulsen atakuwa na kazi ngumu ya kuhakikisha kikosi chake kinaibuka na ushindi ili kurudisha imani ya mashabiki.
Kabla ya kuondoka, Poulsen alisema anakwenda kuandika rekodi mpya akiwa na Stars yenye matumaini ya ushindi.

Stars iliweka kambi jijini Mwanza na Poulsen anaamini kuwa mazingira ya hali ya hewa ya Mwanza yanaoana na ya Uganda kwa wakati huu na kikosi chake kilifurahia mazingira hayo.

Stars leo hii inawakosa washambuliaji wake nyota, Mbwana Samata na Thomas Ulingwengu wanaocheza timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemkokrasi ya Congo.

Mazembe inayomilikiwa na tajiri, Moise Katumbi iligoma kuwaachia Samata na Ulimwengu kwa madai ya kwamba bado wana majukumu kwenye klabu yao.

Kukosekana kwa nyota hao, kutamlazimu Poulsen kuwategemea Mrisho Ngasa na John Boko watakaosaidiana na Simon Msuva.

Safu ya ulinzi itaongozwa na Shomari Kapombe na Kelvin Yondan na hakuna shaka, Mwinyi Kazimoto na Frank Domayo kucheza nafasi ya kiungo.

Kwa mara ya mwisho Stars ilitwaa ubingwa wa michuano ya Chalenji nje ya ardhi ya Tanzania mwaka 1994 ilipowachakaza wenyeji Kenya katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Nakivubo.

No comments:

Post a Comment