Pages

Sunday, October 28, 2012

MVUA KUBWA YALAZA MECHI IRINGA

MVUA kubwa iliyonyesha jana mkoani Iringa imesababisha mchezo wa ligi daraja la kwanza kati ya Polisi Iringa na Mbeya City uliokuwa uchezwa kwenye uwanja wa Samora kuahirishwa.

Akizungumza kwa njia ya simu toka Iringa msimamizi wa kituo hicho Eliud Mvella alisema kuwa mvua imenyesha kwa muda mrefu hali iliyofanya uwanja kujaa maji hivyo usiweze kutumika kuchezea mpira.

"Unajua mpira unatakiwa ukipigwa uzunguke hadi umfikie mchezaji ila kwa hali uwanja ulivyokuwa ilibidi tuliahirisha mchezo ili maji yakauke", alisema Mvella.

Kwenye uwanja wa Kambarage Shinyanga wenyeji timu ya Mwadui waliifunga Polisi Mara mabao 3-0.

Mabao ya Mwadui yalifungwa na Athuman Husein dakika ya saba kwa njia ya penalti, Chuku Chiko akiiipatia bao la pili dakika ya 32 na Mapunda Lulago alifunga bao la tatu dakika ya 46.

Mchezaji Abdallah Abdallah wa Polisi Musoma alionyeshwa kadi nyekundu kwa kutaka kumdanganya mwamuzi kwa kufunga bao kwa mkono kwani kabla alikuwa na kadi ya njano na kuonyeshwa ya pili na kutolewa.

Mpaka mwamuzi Maulid Mwikalo anapuliza filimbi kuashiria mchezo kumalizika Mwadui ambao walikuwa wenyeji walikuwa na mabao 3-0.

Huko uwanja wa Ally Hassan Mwinyi Tabora wenyeji Polisi Tabora walipokea kipigo cha bao 1-0 toka kwa maafande wenzao wa Polisi Dodoma, bao pekee la Juma Omary lililofungwa dakika ya 70.

Uwanja wa Lake Tanganyika wenyeji Kanembwa waliifunga Morani ya Manyara mabao 2-0 na Kurugenzi ya Mufundi ikaifunga JKT Mlale 2-0 mchezo uliochezwa uwanja wa Wambi Makambako.

Uwanja wa Jamhuri Morogoro wenyeji  Burkinafaso walishindwa kuutumia uwanja wao baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 toka kwa Mkamba.

No comments:

Post a Comment