Pages

Wednesday, September 19, 2012

UWANJA WA T.C CHANG'OMBE WAFUNGWA KWA MUDA

UWANJA wa T.C Chang'ombe umefungwa kwa muda wa mwezi mmoja kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo.

Uwanja huo ambao unamilikiwa na kampuni ya Sigara ambao upo Chang'ombe Temeke unafanyiwa matengenezo kwenye sehemu ya kuchezea kwa kuotesha nyasi na kusawazisha.

Akizungumza na HABARI ZA MICHEZO meneja wa uwanja, Edwin Mapunda, alisema wameamua kufunga uwanja huo kwa kipindi cha mwezi mmoja ili kuurudisha kwenye hali yake ya awali.

"Tumefunga uwanja wa muda ili kuufanyia marekebisho kwa kuotesha nyasi na kusawazisha kwa sababu ulikuwa kipara sana na sehemu za goli zilikuwa zimechimbika", alisema Mapunda.

Pia Mapunda alisema kuwa wanajua ni kiasi gani timu zilizokuwa zinatumia uwanja huo zilivyoathirika kwa vile ni kipindi cha ligi lakini hawana namna zaidi ya kuwaommba radhi na kuvumilia kwani ukiwa tayari watarudi

"Tuliwapa notisi timu zinazofanyia mazoezi uwanja wetu lakini tunasikitika kwani imetokea kwa kipindi ambacho ligi imeshaanza hivyo tunawaomba radhi na watuvumilie kwa kipindi hiki kifupi watarejea ukitengemaa", alisema Mapunda.

Timu ambazo zinatumia uwanja huo ni Simba na African Lyon na sasa Simba wanafanyia mazoezi uwanja wa Kinesi uliopo Urafiki Ubungo.

African Lyon wao wamebaki wakitumia sehemu ndogo ambayo hutumika kuchezea timu za watoto.
HABARI ZA MICHEZO lilishuhudia uwanja huo ukiwa umemwagwa mbolea ya samadi na huku ukitifuliwa tayari kuoteshwa nyasi.

No comments:

Post a Comment