Pages

Monday, September 17, 2012

UCHAGUZI WA WANACHAMA WA TFF

 
Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika kikao chake kilichofanyika Septemba 15, 2012 ilijadili michakato ya uchaguzi wa vyama wanachama wa TFF inayoendelea hivi sasa kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa TFF mwishoni mwa mwaka huu. Kamati iliamua yafuatayo;
 
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Njombe (NJOREFA)
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilibaini kuwa uongozi wa muda wa NJOREFA haukutoa ushirikiano wa kutosha kuiwezesha Kamati ya Uchaguzi ya NJOREFA kuanza mchakato wa uchaguzi kwa tarehe kwa tarehe iliyokuwa imepangwa na hivyo kusababisha kuchelewa kuanza kwa mchakato huo wa uchaguzi wa mkoa huo mpya.
 
Kamati imebaini pia kuwa kutokana na changamoto za kiuongozi zinazoukabili mkoa huo mpya, mchakato wa uchaguzi ulioanza Septemba 2, 2012 haukuzingatia kikamilifu Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
 
Kutokana na kasoro hizo za msingi, mchakato wa uchaguzi wa NJOREFA utaanza upya Septemba 18, 2012 ukizingatia Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF. Uchaguzi wa NJOREFA utafanyika Oktoba 28, 2012.
 
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA)
Kamati ilibaini kuwa kuna mkanganyiko katika mchakato wa uchaguzi wa TAREFA na kwamba mkanganyiko uliotokea umesababishwa na Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA kutotimiza wajibu wake wa kusimamia uchaguzi wa TAREFA kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
 
Kutokana na kuvurugika kwa mchakato wa uchaguzi wa TAREFA uliosababishwa na kiwango kikubwa cha ukiukwaji wa Kanuni za Uchaguzi, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imejiridhisha kuwa Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA haina uwezo wa kusimamia majukumu ya uchaguzi wa TAREFA na kuzingatia kikamilifu matakwa ya Kanuni za Uchaguzi ya Wanachama wa TFF.
 
Kwa kuwa Kamati ya Uchaguzi wa TAREFA imeshindwa kutimiza wajibu wake na hivyo kusababisha mkanganyiko na uvurugaji wa uchaguzi wa TAREFA, Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa mamlaka yake yaliyoainishwa katika Katiba ya TFF Ibara ya 49(1) na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF Ibara ya 10(6), 26(2) na (3) imeamua yafuatayo;
 
(i)          Imefuta Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA. Uongozi wa TAREFA unatakiwa kuteua Kamati mpya ya Uchaguzi itakayoandaa na kutekeleza majukumu yake ikizingatia Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF na Katiba ya TAREFA. Uteuzi wa Kamati mpya ya Uchaguzi ya TAREFA ufanyike kabla ya Septemba 24, 2012.
 
(ii)        Imefuta mchakato wa uchaguzi wa TAREFA. Mchakato wa uchaguzi utaanza upya Septemba 25, 2012 na uchaguzi utafanyika Novemba 4, 2012.
 
Vyama vya Mpira wa Miguu mikoa ya Manyara (MARFA) na Kilimanjaro (KRFA)
Uchaguzi wa MARFA na KRFA utafanyika Septemba 22, 2012 kama ilivyopangwa.
 
UTENDAJI WA KAMATI ZA UCHAGUZI ZA WANACHAMA WA TFF
Kamati imebaini baadhi ya viongozi wa vyama vya wanachama wa TFF wanaomaliza muda wao wanashiriki kudhoofisha michakato ya uchaguzi ya vyama vya mpira wa miguu kwa kutotoa fursa kwa Kamati za Uchaguzi za vyama wanachama kuanza michakato ya uchaguzi kwa tarehe zilizopangwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
 
Kwa kuwa ni wajibu wa viongozi waliopo madarakani kuhakikisha kuwa vyama vyao vinafanya uchaguzi kwa mujibu wa Katiba zao na Kanuni za Uchaguzi, Kamati ya Uchaguzi ya TFF haitasita kupendekeza kwa Mamlaka husika za TFF vyama hivyo kuchukuliwa hatua za Kikatiba kwa kushindwa kutimiza matakwa ya Katiba ya TFF kwa kuwa na uongozi ambao muda wa ukomo wa madaraka utakuwa umepita na hivyo kutokidhi matakwa ya Ibara ya 12(2)(a) ya Katiba ya TFF.
 
Kamati ya Uchaguzi ya TFF inavishauri vyama wanachama wa TFF kuzingatia ratiba ya uchaguzi na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF wakati wote wa michakato ya uchaguzi wa viongozi wa vyama vyao. Viongozi walioko madarakani wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa Kamati za Uchaguzi kama ilivyoianishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi.
 
Hamidu Mbwezeleni
Makamu Mwenyekiti
Kamati ya Uchaguzi ya TFF

No comments:

Post a Comment