Changalawe na Rais wa TBF |
Na Rahel Pallangyo
BONDIA wa Tanzania, Yusuf Changarawe amepata medali
ya fedha baada ya kushindwa pambano lake la fainali la mashindano ya kusaka
nafasi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki itakayofanyika Paris, Ufaransa 2024.
Changarawe alipigwa na bondia kutoka Misri,
Abdelrahman Abdelgawwad katika pambano la uzito wa kilo 80 na hivyo kukosa
nafasi ya kuiwakilisha Afrika katika Michezo ya Olimpiki.
Bondia huyo na wengine wa Tanzania sasa watasubiri
mashindano mengine mawili yatakayofanyika Italia na Thailand Februari na Aprili
mwakani ili kusaka tena nafasi ya kwenda Paris katika Olimpiki.
Tanzania katika mashindano hayo ya kufuzu huko
Dakar, Senegal ilipeleka mabondia sita, wanne wa kiume na wawili wa kike, ambao
walikwenda kusaka nafasi ya kwenda Paris.
Mbali na Changarawe, mabondia wengine wa Tanzania ni
Musa Malegesi (kilo 92), Mwalami Salum (kilo 57) na Abdallah Mohamed (kilo 51)
wakati wanawake ni Zulfa Macho (kilo 50) na Grace Mwakamele (kilo 60).
Mkuu wa msafara wa timu hiyo alikuwa Rais wa Shirikisho
la Ndondi Tanzania (BFT), Lukelo Wilillo. Viongozi wengine ni Mashaga (kocha
msaidizi), Samuel Kapunga (Kocha Mkuu) na Aisha George (matroni).
No comments:
Post a Comment