TIMU ya
taifa ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kesho inatarajia kushuka katika dimba la
Uhuru, Dar es Salaam kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya timu ya
Taifa ya Malawi.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo, Kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga alisema
wamejiandaa vema kwani anaamini mchezo utakuwa na ushindani kwa sababu Malawi
wamewaita nyota wake wanaocheza soka nje ya nchi yao.
“Tunataka
ushindi ili tuzidi kupanda katika viwango vya FIFA hadi tufike kwenye tarakimu
mbili, najua mchezo utakuwa na ushindani lakini tumejiandaa kushinda,” alisema
Mayanga.
“Wamebadilisha
kikosi kwa kiasi kikubwa, kwa maana hiyo hatupaswi kuwadharau licha ya matokeo
mazuri tuliyopata dhidi yao kwenye mechi za COSAFA,” alisema Mayanga ambapo
Taifa Stars iliifunga mabao 2-0 katika mchezo huo
Naye nahodha
wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ameonyesha kujiamini
na kuwataka Watanzania kwenda uwanjani wakiwa na uhakika wa kufurahi.
“Watanzania waje uwanjani, wengine watutazame
kwenye televisheni wakiwa na uhakika timu yao itapata ushindi kesho (leo),”.
“Wachezaji
wote wana morali na viwango vyao mazoezi ni vikubwa, na cha zaidi
nawahakikishia mimi binafsi nipo kwenye kiwango bora kabisa,” alisema Samatta.
Naye kocha
wa Malawi, Ronny Van Geneugden alisema anaifahamu Taifa Stars kwasababu
walicheza nayo kwenye mashindano ya COSAFA hivyo wamejiandaa kurudisha kipigo
walichopata Afrika Kusini.
“Nimeshaifahamu
Tanzania na namna timu za Afrika zinavyocheza hivyo safari hii tutalipiza
kisasi baada ya kutufunga katika mashindano ya COSAFA,” alisema Van Geneugden
Mbeligiji huyo ambaye alianza kuifundisha Malawi Aprili mwaka huu.
Katika
viwango vya Fifa vilivyotoka mwezi uliopita Malawi inashika nafasi ya 116 na
Tanzania inashika nafasi ya 125.
No comments:
Post a Comment