Bodi ya Ligi (TPLB) ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, limewapiga marufuku makocha watano wa timu za Ligi Daraja la Kwanza kukaa katika mabenchi ya timu hizo kwa sababu ya kukosa sifa.
Makocha hao ni Mathias Wandiba wa Pamba FC ya Mwanza, Salum Waziri wa JKT Mgambo ya Tanga, Adam Kipatacho wa African Lyon ya Dar es Salaam, Omba Thabit wa Mvuvumwa FC ya Kigoma na Ngelo Manjamba wa Polisi Dar.
Makocha hao wamekuwa kwenye mabenchi ya timu wakifanya kazi kama makocha wakuu katika mechi nne mfululizo za Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2017/2018 inayoendelea hivi sasa.
Kwa mujibu wa kanuni ya 72 (3) (5) ya Ligi Daraja la Kwanza, Kocha Mkuu anatakiwa kuwa na Leseni ya chini kuanzia daraja C ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) wakati Kocha Msaidizi anatakiwa kuwa na sifa isiyopungua ngazi ya Kati cha Ukocha (Intermediate).
Tayari Idara ya Ufundi ya TFF imefafanua wazi kuwa makocha hao hawana Leseni C ya CAF hivyo hawastahili kukaa kwenye mabenchi ya timu zao kama makocha wakuu.
Vitendo vinavyofanywa na timu husika ni ukiukwaji wa kanuni, na ni matarajio ya TFF kuwa viongozi wa timu hizo watasitisha mara moja kwa makocha hao kukaa kwenye mabenchi ili kuepika adhabu.
TFF tunachukua nafasi hii kuzikumbusha klabu husika kwamba kuanzia msimu ujao 2018/2019 kuwa sifa ya Kocha Mkuu wa kila timu ya Daraja la Kwanza ni Leseni B ya CAF.
No comments:
Post a Comment