Kamati ya Bodi ya Uendeshaji na Kusimamia Ligi (Kamati ya Saa 72),
iliketi mwishoni mwa wiki iliyopita na kupitia mchezo mmoja baada ya
mwingine na kuibuka na uamuzi ufuatao.
Mechi namba 212 (Yanga 2 Vs Kagera Sugar 1). Kamati imefuta kadi
nyekundu ya moja kwa moja aliyopewa mchezaji Mbaraka Yusuf wa Kagera
Sugar baada ya kubaini hakutenda kosa lililosababisha mwamuzi ampe
adhabu hiyo. Uamuzi huo umefanywa kwa mujibu wa Kanuni ya 9(8) ya Ligi
Kuu.
Pia Mwamuzi wa mechi hiyo, Ngole Mwangole ameondolewa kuchezesha Ligi
Kuu ya Vodacom kwa vile uamuzi aliofanya haukuwa sahihi. Hatua dhidi ya
Mwamuzi Mwangole imechukuliwa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(1a) ya Ligi
Kuu.
Hii ni mara ya pili kwa Ngole kushindwa kutafsiri sheria uwanjani
kwani katika duru la kwanza alionywa baada ya kukataa bao JKT Ruvu
ilipocheza na Mtibwa Sugar katika Ligi Kuu ya ismu huu wa 2016/17.
Mechi namba 214 (JKT Ruvu 2 Vs Azam 2). Klabu ya Azam FC imepigwa
faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kutoingia vyumbani, na
badala yake kukaa nje. Kitendo hicho ni kwenda kinyume na Kanuni ya
14(13) ya Ligi Kuu, na adhabu imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48)
ya Ligi Kuu.
Mechi namba 215 (Mbao FC 1 Vs Tanzania Prisons 0). Mchezaji Jeremiah
Juma wa Tanzania Prisons amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh.
500,000 kutokana na kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumpiga ngumi
mpinzani wake. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(3) ya
Ligi Kuu.
Pia timu ya Tanzania Prisons imeagizwa kurudisha mpira uliochukuliwa
na mshabiki wake baada ya kumalizika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 16,
2017 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Msimamizi Msaidizi wa Kituo cha Mwanza aliripoti kwa Meneja wa
Prisons, Bw. Enock Mwanguku tukio la shabiki huyo aliyechukua mpira huo
na kuingia kwenye gari la timu hiyo. Meneja huyo aliahidi kufuatilia,
lakini hadi timu yake inaondoka uwanjani hakutoa mrejesho wowote.
Mechi namba 220 (Majimaji 3 Vs Mwadui 0). Klabu ya Majimaji imepigwa
faini ya sh. 500,000 kutokana na timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia
mlango usio rasmi. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi
Kuu.
Mechi namba 224 (Yanga 2 Vs Tanzania Prisons 0). Klabu zote zimepigwa
faini ya sh. 500,000 kila moja kwa timu zao kutoingia vyumbani na
kusababisha wachezaji wakaguliwe wakiwa nje ya vyumba. Adhabu hiyo ni
uzingativu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.
No comments:
Post a Comment