WIKI
iliyopita tulishuhudia mechi kali Ulaya, ambapo miamba ilikuwa ikipambana
kutafuta kufuzu kuingia nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
Waliovuka
wamefanya hivyo, hata kama ni kwa malalamiko ya waliokwama, na sasa tutasubiri
kuina nusu fainali. Wakati tukisubiri hayo, tunaendelea kusawiri ni wachezaji
gani vijana walio mahiri sana kwa sasa Ulaya hii hii.
Niklas
Sule (Hoffenheim, 21, Mlinzi)
Kwa kawaida
ukiona Bayern Munich wamemfuata mchezaji na kumng’ang’ania katika soka ya
Ujerumani basi ujue hicho kweli ni kifaa. Miamba hawa wa Ujerumani walijihisi
kwamba walitakiwa kuisaka kwa udi na uvumba saini ya Niklas Sule kwa ajili ya
msimu ujao, na tayari wameshafanya hivyo.
Wanadaiwa kumfunga
mkataba wa muda mrefu kwa thamani ya pauni milioni 21.68, Ni rahisi kuona
sababu; akiwa na umri wa miaka 21 tu tayari Sule amejiongeza kuwa mmoja wa
walinzi bora zaidi wa kati katika Bundesliga.
Kocha wa
Timu ya Taifa ya Ujerumani, Joachim Low hakushindwa kumuona na tayari
amemchezesha kimataifa wakati katika ngazi ya klabu Sule ametoa mchango mkubwa
kwa Hoffenheim kujisukuma kuendea nafasi za juu za ligi kuu.
Sule ni
mbichi, akiwa na sehemu ya kuongeza vitu bado kwa ajili ya kujiboresha yeye na
timu atakazokuwa nazo; ni aina ya mlinzi wa kisasa anayeonesha mahaba kwa mpira
kuwa mguuni pale lakini pia ni mzuri angani na ana nguvu za miguu na kichwa na
anafaa kwa mfumo wa kocha yeyote yule.
Alexander
Isak (Borussia Dortmund, 17, Mshambuliaji)
Uliza
mshambuliaji yeyote ni mshambuliaji gani wangependa kufananishwa naye, basi
Zlatan Ibrahimovic atakuwa juu miongoni mwao. Alexander Isak anatambulika
katika Ujerumani kama ‘The Zlatan’ mpya. Alilazimisha kuingia kikosi cha kwanza
akiwa na umri wa miaka 16 tu na alipofikisha umri wa miaka 17 alikuwa anaongoza
mstari wa mashambulizi akiwa na AIK, akafunga bao dakika ya 15 tu siku yake ya
kuzaliwa.
Uwapo wake
uwanjani unasikika sana, yupo vizuri akiwa na mpira na muda wote hufungua
vyumba tayari kuupokea. Mchezaji huyu aliyezaliwa Sweden na wazazi raia wa
Eritrea ni mmaliziaji mzuri ambaye mwaka jana alifunga mabao 10 akiwa Ligi Kuu
ya Sweden. Haikushangaza kuona kwamba Real Madrid ni moja ya klabu zilizomtaka
ila ameamua kuwa na Dortmund mwaka huu, na amefanya vyema kwani atapata muda
zaidi wa kucheza.
Sandro
Ramirez (Malaga, 21, Mshambuliaji)
Ikiwa
Alexander Isak anataka uthibitisho kwamba alifanya uamuzi sahihi, amtazame tu
Sandro Ramirez. Mshambuliaji huyu Mhispaniola alipanda kutoka Akademia ya
Barcelona – La Masia – lakini akaachwa tu akizurura kutokana na marufuku ya
usajili waliyowekewa.
Kiangazi
kilipofika aliamua kuondoka akajiunga na Malaga akiwa mchezaji huru na mambo
yamemwendea vizuri kabisa. Katika mechi 19 amefunga mabao saba kwenye Ligi Kuu
ya Hispania, ameiva vile ambavyo Barcelona wangependa.
Angeweza
kuingia Ligi Kuu ya England (EPL) maana tayari Kocha wa Tottenham Hotspur,
Mauricio Pochettino alimuwinda mara kadhaa. Huenda Malaga wakikubali Pochettino
angemchukua kiangazi kijacho.
Morgan
Sanson (Marseille, 22, Kiungo)
Kifaa
kilichosukwa hasa hiki na kimekuwa kkipamba vichwa vya habari, ikiwa ni zaidi
ya Dimitri Payet aliyesajiliwa kutoka West Ham. Utampenda ukimwona anavyocheza
kwenye Uwanja wa Stade Velodrome.
Sanson ameshacheza
mechi 146 kwenye timu ya wakubwa kwa umri wake huo mdogo tu na kwa hakika ni
mtu mwenye ubunifu mkubwa. Marseille walimpata kwa euro milioni tisa tu.
Alikuwa mchezaji wa kwanza katika Ligue 1 ya Ufaransa kutoa usaidizi kwa mabao
10 msimu huu,idadi kubwa kwa kiungo wa kati.
Kila wiki
anazidi kuwa bora kwa klabu yake ambapo kwa wiki tano kwenye mechi sita ama
amefunga bao au kutoa usaidizi kwa jamaa hawa wanaojulikana kwa jina la utani
la Les Phoceens.
Jose
Luis Gaya (Valencia, 21, Beki wa Kushoto)
Manchester
City wana matatizo kwenye ngome yao na moja ya suluhu kwao ingekuwa kumpata mtu
wa aina ya Jose Luis Gaya. Ni beki mwenye akili ya kushambulia na amewasaidia
sana Valencia katika La Liga.
Gaya ana
kasi lakini licha ya umbo lake dogo amekuwa akiwazidi kimsuli mawinga wakubwa
kwa umbo. Kuna uwezekano mkubwa kabisa kwa Gaya kuwa mzuri zaidi lakini tayari
ameonesha vitu adimu na Pep Guardiola anaweza kuwa kocha mwenye kumhitaji na
kumfaidi zaidi, ambapo ana uwezo wa kuwaimarisha walinzi wadogo kuwa bora
kabisa duaniani.
Giovanni
Simeone (Genoa, 21, Mshambuliaji)
Kuingia
Ulaya kunaweza kuwa kugumu kwa mchezaji mdogo, lakini huweza kumsaidia ikiwa
ana familia huku. Hii ndiyo hali aliyo nayo Giovani ‘Cholito’ Simeone, mwana wa
Kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone.
Someone
alionesha uzuri wake mapema msimu huu alipofunga bao dhidi ya mabingwa wa
Italia, Juventus na kuwapa Genoa ushindi murua sana uliofurahiwa. Amefunga
mabao 10 katika mechi 20 alizocheza hadi naandika mhaya.
Hii maana
yake ni kwamba anaanza kuwavuta klavu kubwa kutoka nchi mbalimbali, ikiwa ni
pamoja na England, kumtaka. Ana nguvu sana, mchezo mzuri lakini pia anajua cha
kufanya wakati hana mpira. Inaelezwa kwamba Everton wanalenga kumsajili, lakini
hata kama si kweli huu ni mwanzo tu wa mshambuliaji anayetarajiwa kuwa mahiri
kuliko hata baba yake. ITAENDELEA.
No comments:
Post a Comment