Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Saturday, December 31, 2016

SIMBA, YANGA NA AZAM FC KUENDELEZA UBABE MAPINDUZI?


UHONDO wa soka sasa unahamia visiwani Zanzibar ambapo vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga zitapambana kuwania ubingwa wa Kombe la Mapinduzi lililoanza kutimua vumbi jana kwa timu ya Taifa Jang'ombe dhidi ya ndugu zao, Jang'ombe Boys.

Hata hivyo, ukiachana na mechi hiyo, kitimutimu kitaanza rasmi kesho kwa mchezo kati ya mabingwa watetezi, URA ya Uganda  dhidi ya KVZ kuanzia saa 10:00 jioni kabla ya Simba kumenyana na Taifa ya Jang'ombe saa 2:30 usiku.

Mechi za Kundi B zitaanza Jumatatu kwa Azam FC kumenyana na Zimamoto kuanzia saa 10:00 jioni kabla ya Yanga kumenyana na Jamhuri saa 2:30 usiku.

Yanga itashuka dimbani bila ya beki wake raia wa Togo, Vincent Bossou ambaye ana majukumu ya timu yake ya taifa  iliyo kwenye maandalizi ya mwisho ya kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) inayotarajiwa kuanza Januari 14  nchini Gabon ambapo Togo ilikata  tiketi ya kushiriki michuano hiyo baada ya kuinyuka Djibouti  mabao 5- 0.

Kwa mujibu wa Katibu mkuu wa Yanga, Baraka Deusdetit, kikosi hicho cha Yanga kitaondoka alasiri leo kikiwa na wachezaji 26 na benchi zima la ufundi baada ya mazoezi yao ya mwisho asubuhi watakayofanya kwenye uwanja wa Uhuru.

Kikosi kamili cha Yanga kinachokwenda Zanzibar ni makipa: Deogratius Munishi 'Dida', Benno Kakolanya na Ali Mustafa 'Barthez'.

Mabeki ni Nadir Haroub 'Cannavaro', Pato Ngonyani, Vincent Andrew, Hassan Kessy, Mwinyi Hajji, Kelvin Yondan, Juma Abdul na Oscar Joshua.

Viungo ni Haruna Niyonzima, Justin Zulu, Simoni Msuva, Juma Mahadhi, Geoffrey Mwashiuya, Deus Kaseke, Saidi Juma 'Makapu', Thabani Kamusoko na Yussuf Mhilu.

Washambuliaji ni Donald Ngoma, Amisi Tambwe, Emmanuel Martin, Obrey Chirwa na Matheo Anthony.

Kwa upande wa Simba wanaondoka kikosi kizima kikiongozwa na nahodha Jonas Mkude, mlinda mlango Daniel Agyei, Javier Bukungu, Mohamed Hussein, Abdi Banda, Method Mwanjali, Shiza Kichuya, Mwinyi Kazimoto, Muzamiru Yassin, James Kotei, Pastory Athanas, Mohamed Ibrahim, Peter Manyika, Hamad Juma, Novatus Lufunga, Juma Luizio, Said Ndemla, Moses Kitandu na Laudit Mavugo.

Simba pia itamkosa beki wake Juuko Murshid ambaye pia yupo kwenye kikosi cha Uganda kinachokwenda Ufaransa kujiandaa na michuano ya Afcon.

Wakati Azam ambayo itaanza harakati zake kesho, itaondoka leo pia na itamenyana na Zimamoto katika mchezo utakaofanyika saa 10 alasiri kesho.

Yanga imepangwa kundi B  katika michuano  hiyo ya kila mwaka ikiwa na  Azam FC ya Dar es Salaam, Jamhuri na Zimamoto zote za Zanzibar.

Katika michuano hiyo inayotarajiwa kufanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar kuanzia jana Desemba hadi Januari 13, Kundi A lina timu za Simba, Taifa ya Jang’ombe, Jang’ombe Boys, KVZ na mabingwa watetezi, URA ya Uganda.

Simba, Yanga na Azam zinakwenda kwenye michuano hiyo zikiwa kwenye tatu bora katika msimamo wa Ligi Kuu bara ambapo Simba inaongoza kwa tofauti ya pointi nne dhidi ya Yanga yenye pointi 40 na Azam ina pointi 30.