MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga, kesho wanashuka tena kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kucheza na JKT Ruvu.
Yanga inashuka dimbani ikiwa inaongoza
katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kushinda mechi zake mbili na kujikusanyia
pointi zote sita huku ikifunga mabao matano.
Katika mchezo wa kwanza, Yanga ilishinda
Wagosi wa Kaya Coastal Union kwa mabao 2-0 kabla ya kuibuka na ushindi mwingine
wa mabao 3-0 dhidi ya Prisons ya Mbeya.
Timu hiyo itacheza mechi nne mfululizo
kwenye uwanja wake wa nyumbani kwani baada ya mchezo wa leo, itashuka tena
dimbani kumenyana na watani zao wa jadi Simba Septemba 26 kabla ya kuanza
kutoka wakati itakapocheza na Mtibwa Sugar Septemba 30 kwenye Uwanja wa Jamhuri
Morogoro.
Yanga inahitaji ushindi katika mchezo huo
ili iweze kuzidi kukalia kiti hicho na kufanya biashara mapema kabla ya
kuhesabu mapato jioni.
Yanga imeshafunga mabao matano katika
mechi mbili na haijafungwa bao hata moja, hivyo inaonesha jinsi safu yake ya
ushambuliaji kama akina Donald Ngoma, Hamisi Msuva, Amiss Tambwe na wengineo
ilivyo na uchu wa mabao, hivyo mabeki wa maafande wa JKT Ruvu watakuwa na
kibarua kigumu cha kuwazuia wasifunge.
Hata hivyo, kikosi cha JKT Ruvu
kinachofundishwa na mchezaji na kocha wa zamani wa Yanga, Fred Minziro
hakitakubali kufa kikondoo, kwani kinazihitaji sana pointi hizo tatu ili
kurejesha matumaini ya kufanya vizuri.
JKT Ruvu ndio inaburuza mkia baada ya
kufungwa mechi zote mbili za mwanzo na kuifanya kuwa na kazi kubwa ya kufanya
ili kutoka na pointi zote tatu au moja kwa kutoka sare.
Kocha wa JKT Ruvu, Minziro alikiri kuanza
vibaya kwa ligi hiyo lakini alisema leo hawatakubali kufungwa licha ya uimara
wa Yanga ambayo ina wachezaji wengi wazuri, wakiwemo wa kutoka nje ya nchi.
Alisema kuwa timu yao ilianza vibaya
mechi mbili za mwanzo baada ya wachezaji wake kutokuwepo katika maandalizi ya
mwisho baada ya kuwa katika mashindano ya majeshi nchini Uganda kwa takribani
siku 11.
Pia alisema timu yake ina majeruhi
wawili, lakini alikuwa na imani siku zinavyokwenda timu hiyo itazidi kuimarika
na kufanya vizuri katika mechi zao zijazo.
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub alisema
kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaondoka na pointi zote tatu ili kuzidi
kung’ara katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 16.
Mechi zingine leo ni Stand United
watachea na African Sports katika mchezo utakaofanyika kwenye uwanja wa
Kambarage mjini Shinyanga, huku Mgambo Shooting itawakaribisha wana Lizombe
Maji Maji ya Songea katika uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Mbeya City wenyewe watakuwa wageni wa
ndugu zao wa Tanzania Prisons katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Wakati Mbeya City ni ya nane baada ya
kuwa na pointi tatu kutoka katika mechi mbili walizocheza, Tanzania Prisons
wenyewe ni wa pili kutoka mkiani wakiwa hawana pointi hata moja baada ya
kuchapwa mechi zote mbili za mwanzo.
Mechi hizo zitaendelea tena kesho
Jumapili kwa Mwadui ya Shinyanga kuikaribisha Azam FC huku kocha wa wenyeji hao
Jamhuri Kihwelu kutamba kuibuka na ushindi.
Mtibwa Sugar watacheza na Ndanda FC
katika mchezo utakaofanyika kwenye uwanja wa Manungu, Turiani wakati Simba
baada ya kuanza kwa kucheza mechi mbili ugenini, kesho kwa mara ya kwanza
itakuwa kwenye Uwanja wa Taifa ikicheza na Kagera Sugar.
African Sports wenyewe watakuwa mwenyeji
wa Toto Africans ya Mwanza katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa
Mkwakwani Tanga.
No comments:
Post a Comment