SHIRIKISHO la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)
limeipa Tanzania mgawo wa tiketi 260 za Fainali za Kombe la Dunia nchini
Brazil.
Akizungumza na wandishi wa habari, Ofisa Habari wa
Shirikisho la Soka nchini (TFF) Boniface Wambura, alisema kuwa watanzania
wanaohitaji tiketi hizo wanatakiwa kutuma maombi TFF kwa maandishi wakielezea
aina ya tiketi na mechi wanazotaka kushuhudia.
Pia alisema kuwa hakuna tiketi zitakazoombwa FIFA bila
kuwepo maombi kwa maandishi hivyo wanatakiwa kuchangamkia fursa hii mapema
kwani kuna uwezekano tiketi zote zilizotengwa kwa Tanzania zisipatikane
Tiketi zilizopo kwa Tanzania ni ifuatavyo; kwa hatua
ya makundi (ukiondoa mechi ya ufunguzi), raundi ya 16 bora, robo fainali na
mechi ya kutafuta mshindi wa tatu ni 250.
Kwenye mechi ya ufunguzi, nusu fainali mbili na
fainali (mechi namba 1, 61, 52 na 64) ni tiketi kumi tu zitakazopatikana na bei
za tiketi ziko katika viwango vitatu tofauti.
Mechi ya ufunguzi tiketi zake ni dola za Marekani 495,
330 na 220. Hatua ya makundi (mechi namba 2-48) ni dola 175, 135 na 90. Hatua
ya 16 bora (mechi namba 49-56) ni dola 220, 165 na 110.
Robo fainali (mechi namba 57-60) ni dola 330, 220 na
165 wakati nusu fainali (mechi namba 61 na 62) ni dola 660, 440 na 275. Mechi
ya mshindi wa tatu ni dola 330, 220 na 165. Kiingilio kwa fainali kitakuwa dola
990, 660 na 440.
Wambura alisema TFF itawasilisha maombi ya tiketi hizo
FIFA kuanzia Desemba 8 mwaka huu hadi Februari 7 mwakani na idadi ambayo
itaombwa FIFA itatokana na Watanzania waliowasilisha maombi TFF kwa vile
zinaweza zisipatikane tiketi zote hizo zilitengwa kwa Tanzania.
No comments:
Post a Comment