Bayern Munich imerejea katika kilele cha ligi kuu ya nchini Ujerumani Bundesliga baada ya Bayer Leverkusen
kuchukua usukani kwa muda wakifaidika na goli hewa dhidi ya Hoffenheim
siku ya Ijumaa.
Katika mchezo wa kuvutia hiyo jana Jumapili kati ya Hamburg SV na VFB
Suttgart, vigogo hivyo vya soka la Ujerumani vilitoshana sare ya mabao
3-3.
Na katika mchezo wa mwisho jana jioni uliofikisha mchezo wa roundi ya 9
ya Bundesliga , Wolfsburg ilishinda baada ya kuonesha mchezo dhaifu
katika kipindi cha kwanza dhidi ya Augsburg na kujipatia points tatu za
kwanza ugenini. VFL Wolfsburg ilipata ushindi wa mabo 2-1.
Mabingwa watetezi wa Bundesliga Bayern Munich walirejea kileleni mwa
ligi hiyo wakiipora nafasi hiyo kutoka kwa Leverkusen. Kikosi cha
Leverkusen kilifadika na bao hewa la Kießling siku ya Ijumaa dhidi ya
Hoffenheim. BVB , Borussia ilipata ushindi wa taabu wa bao 1-0 dhidi ya
Hannover kama ilivyokuwa kwa Schalke 04 ambao walikuwa wageni wa wageni
katika ligi hiyo Braunschweig ambao Schalke ilipata ushindi wa kubana wa
mabao 3-2.
Nürnberg na Freiburg zilitoshana sare ya bao 1-1, lakini bado
zimeshindwa kupata ushindi. Siku ya Jumamosi Hertha BSC Berlin
iliishinda Gladbach kwa bao 1-0 na kuchupa hadi nafasi ya nne.
Kwingineko katika bara la Ulaya ,
Mabingwa wa La Liga ligi ya Uhispania Barcelona walishindwa kuuona wavu
siku ya Jumamosi kwa mara ya kwanza katika michezo 65 iliyocheza baada
ya kutoka sare ya bila kufungana na Osasuna.
Atletico Madrid ikakubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Espanyol wakati
Real Madrid iliibuka kidedea kwa kupata ushindi wa tisa mfululizo.
Fiorentina iliirarua Juventus Turin kwa mabao 4-2 baada ya kuwa nyuma
kwa mabao 2-0, na kuipa Juventus kipigo chake cha kwanza msimu huu
katika Serie A nchini Italia.
AS Roma nayo ikainyoa bila maji SSC Napoli kwa mabao 2-0.
Nchini Uingereza Arsenal London imeongeza uzito katika kampeni yake ya
kuwania ubingwa msimu huu baada ya kuweka wavuni mabao 4 dhidi ya
Norwich City wakati mchezaji wa kati Mesut Ozil akionesha uwezo mkubwa
wa kuiunganisha timu hiyo. Arsenal iko points mbili juu ya msimamo wa
ligi ikifuatiwa na Chelsea.
Manchester City na Tottenham Hotspurs zilipata ushindi mwishoni mwa
juma, lakini hali ya wasi wasi inawakumba mabingwa watetezi Manchester
United baada ya kushindwa kupata kama kawaida yao ushindi wa kufuatana
na kuiacha timu hiyo ikiwa katika nafasi ya nane.
Champions League
Kinyang'anyoro cha Champions League kinarejea uwanjani kesho Jumanne na
Jumatano.
Arsenal ya London na Barcelona ni timu mbili ambazo zinawania
kupata ushindi wa tatu katika michezo mitatu ya makundi yao.
Viongozi hao wa Premier League Arsenal na Borussia Dortmund makamu
bingwa wa Champions League walikabiliana katika msimu wa mwaka 2011-2012
wakati Robin van Persie alipofanikisha ushindi wa Arsenal nyumbani.
Mchezo wa pili ulikuwa sare ya bao 1-1 mjini Dortmund.
Schalke 04 pia itakuwa uwanjani kesho Jumanne ikioneshana kazi na
Chelsea London . Chelsea inahitaji kwa udi na uvumba ushindi mjini
Gelsenkirchen kupata kujiamini zaidi baada ya ushindi wao wa mabao 4-0
dhidi ya Steaua Bucharest katika kundi E. Michezo mingine ni kati ya
Steaua Bucharest ikiikaribisha Basel ya Uswisi, Marseille ya Ufaransa
inakuwa mwenyeji wa SSC Napoli ya Italia, wakati katika kundi G , Porto
ya Ureno imewaalika Zenit St Petersburg ya Urusi.
Austria Vienna ina
miadi na Atletico Madrid , na Celtic itakuwa kibaruani na Ajax Amsterdam
ya Uholanzi katika kundi H, ambapo pia AC Milan inaikaribisha nyumbani
Barcelona.
Michezo hiyo inaendelea siku ya Jumatano ambapo mabingwa Bayern Munich
inawakaribisha Pilsen ya Denmark na Leverkusen wako nyumbani
kuikaribisha Schachtar Donetzk ya Ukraine.
No comments:
Post a Comment