PALE Jordi Alba alipofunga bao la kufutia machozi dhidi ya Real
Madrid kwenye Copa del Rey, lilionekana halina umuhimu.
Licha ya Barcelona kuongoza La Liga kipindi hicho kwa tofauti
kubwa ya pointi, kitu kilichowapa ubingwa, lakini Real Madrid walionekana
kushika utawala kwenye mechi kati yao.
Kiukweli wakati wa kukumbukwa kwenye historia ya El Clasico, katika
miaka ya karibuni ni sare ya mabao 2-2 kwenye Copa del Rey msimu wa 2011-12,
hii ilikuwa siku ambayo Madrid walitoka nyuma kwa mabao 2-0 kwenye uwanja wa Camp
Nou, lakini bado walitolewa kutokana na kupoteza mechi ya kwanza.
Wakati wakisaka kusawazisha mabao hayo, vijana wa Jose
Mourinho walionyesha sura yao nyingine na walifanikiwa na iliwapa kujiamini
kulikohitajika kucheza na kikosi bora cha Barca na kuanza kuona kumbe
wanafungika.
Tangu walipopata sare hiyo Januari 2012, Madrid wameshinda
mechi nne kati ya saba dhidi ya Barca, huku wakitoa sare mbili na kufungwa mara
moja tu.
Licha ya Barcelona kuchukua La Liga msimu huu, lakini
ilionekana wazi kuwa utawala wa Madrid Hispania ulikuwa umerudi. Vichapo
walivyovipata wote wawili kutoka kwa miamba ya Kijerumani, vilizifanya klabu
zote mbili kuchanganyikiwa na kujipanga upya.
Na hii inaweza kuwa faida kwa El Clasico.
Barca imeshuka kiwango msimu huu, na kubadili wachezaji ni
jambo muhimu sana kwao wakati huu wa kiangazi.
Neymar tayari ameshatua kutoka Santos, kipa anakaribia kutua
kwenye klabu hiyo kutokana na ukweli kwamba, Victor Valdes anajiandaa kusepa Monaco.
Hakuna siri kuwa wanahitaji mabeki wengine na viungo.
Cha muhimu ni kwamba, falsafa yao ya soka haibadiliki, kwa
sababu miguu iliyochoka baada ya misimu mitano ya utawala haionyeshi kuishiwa
mbinu.
Madrid kutakuwa na mabadiliko makubwa, kuanzia kwa ujio wa Carlo
Ancelotti, kumrithi Mourinho, anataka Fabio Cannavaro ndiye awe msaidizi wake.
Dani Carvajal atarudi kuwania namba na Alvaro Arbeloa, beki ya
kulia, wakati Ancelotti akitizamiwa kuleta namba tisa mwingine; Edinison
Cavani, Luis Suarez, Robert Lewandowski na Sergio Aguero wanahusishwa na klabu
hiyo.
Pia kuna suala la Gareth Bale na Isco wote hawa, wanatajwa
kutua Santiago Bernabeu.
Inaonekana kana kwamba Madrid watakuwa bize zaidi kama wakati
wa kiangazi mwaka 2009 walipowaleta kina Cristiano Ronaldo, Kaka, Xabi Alonso na
Karim Benzema na wengine kibao.
Hii yote inaelekeza kidole kwenye zama mpya za hadithi ya El
Clasico; vitu vingi vinahitajika na inasisimua kuanza ukurasa mpya.
Kulikuwa na shaka pale Pep Guardiola, alipoondoka baada ya
kuchoshwa na presha na vita ya maneno na Mourinho, kitu ambacho mwenyewe
alikikanusha alipoondoka, japokuwa alikiri kuchoka na alihitaji kupumzika.
Guardiola alisema kwamba, Mourinho hakumsababisha apumzike
soka, bali alikuwa amechoshwa na kazi za kila siku na kushinda.
Kama Guardiola hakuwa amechoshwa na ugomvi na maneno ya kila
kukicha ambayo yalikuwa yakizidi kati ya makocha, wachezaji, vyombo vya habari
na mashabiki wa timu hizo mbili, kutokana na kucheza mara kwa mara, wakati yeye
na Mourinho walipokuwa wakiziongoza timu hizo mbili kubwa, basi kuna baadhi ya
wachambuzi wanaamini dunia ilikuwa imewachoka.
Kulikuwa na mechi sita za El Clasico mwaka 2012 na saba mwaka
mmoja kabla, timu hizo zimekutana mara 16 tangu mwaka 2011.
Pamoja na msisimko na ubora ambao mechi hizi zilikuwa nazo,
lakini kitendo cha sura zile zile kuhusika kwenye mechi hizi kilianza
kuwachosha watu; Kiangazi mwaka huu timu hizo zinatakiwa kuongeza sura mpya.
Ancelotti alikiongoza kikosi cha PSG dhidi ya Barca, kwenye
uwanja wa Camp Nou na walifanikiwa kupata bao la kuongoza kabla ya kuruhusu bao
na kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa sheria ya goli la ugenini.
Matumaini ni kuwa Ancelotti atafanya usajili kama akipewa
majukumu ya kuinoa Real Madrid.
Huku Tito Vilanova akiwa na muda wa kukisuka upya kikosi cha Barcelona
kiendane zaidi na mapenzi yake, bila kusahau kuondoka kwa Mourinho, ni wazi
sasa El Clasico itarudi kuchezwa uwanjani na siyo nje ya uwanja kama zama za
Mourinho.
Na hili ndilo jambo ambalo kila mtu atafurahi kuliona kuliko
kukaa na kusikiliza kelele zisizoisha za nje ya uwanja.
No comments:
Post a Comment