Simon Msuva (katikati) akiwa na Haruna Niyonzima kulia na aliyepo kushoto ni Frank Domayo |
WAKATI timu ya Simba ikibaki na matarajio ya kuwafunga watani wao wa
jadi Yanga, ili iendeleze heshima baada ya kuukosa ubingwa, benchi la ufundi la
timu hiyo limeelekeza mafunzo maalum kwa mabeki wa timu hiyo, ili kukabiliana
na mashambulizi ya wapinzani hao hasa kumzuia kiungo wake hatari chipukizi
Simon Msuva.
Katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye uwanja wa Kinesi
Ubungo jijini Dar es Salaam juzi na jana, kocha mkuu wa timu hiyo, Patrick
Liewig alionekana kuwa makini zaidi na
wachezaji wa safu ya ulinzi.
Akizungumza jijini kocha huyo, alisema amekuwa akikiandaa kikosi
chake katika kila idara, lakini kwa sasa anaangalia zaidi sehemu ya ulinzi
kutokana na umuhimu wa mechi zinazowakabili mbele yao.
Alisema, mechi yao ya kesho itakayowakutanisha na timu ya Ruvu
Shooting, wanaipa nafasi kubwa kwa vile wanafahamu timu hiyo iliyopo kwenye
nafasi ya saba katika msimamo wa ligi, ina kiwango kizuri na imeonekana kuwa
tishio kwenye michuano hiyo.
Katika hatua nyingine Liewig alisema vilevile anaiandaa safu ya ulinzi
kutokana na matayarisho ya mechi yao ya mwisho dhidi ya Yanga, itakayochezwa
Mei 18 jijini Dar es Salaam.
Bila kutaja jina la mshambuliaji anayewapa kiwewe, kocha huyo
alisema, anaamini itakuwa ngumu kuliko
zote kwa vile timu hiyo ina safu ya washambuliaji vijana na wenye kasi hivyo
wanahitaji kuwa na mabeki imara.
Yanga hadi sasa inajivunia washambuliaji wake chipukizi akiwemo Frank
Dumayo na Simon Msuva, hivyo tahadhari hiyo ya Liewig inaonyesha kuwahofia
zaidi washambuliaji hao.
Hata hivyo Simba kesho inajitupa kwenye Uwanja wa Taifa kucheza na
Ruvu Shooting ikiwa inawania pointi tatu ili iweze kuisogelea Kagera Sugar
iliyopo nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 40.
No comments:
Post a Comment