KIMENUKA! Hilo ndilo neno unaloweza
kuanza kulitamka wakati ukielezea hofu kubwa ya wachezaji nyota wa Arsenal
ambao wamebaini kuwepo mpasuko katika chumba chao cha kubadilishia kati ya
Kocha Mkuu, Arsene Wenger na Msaidizi wake, Steve Bould.
Hali hiyo imebainika katika mechi ya
Kombe la Ligi maarufu kama 'Capital One Cup' dhidi ya Bradford ambapo timu hiyo
ilitolewa kwa penalti 3-2 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120.
Licha ya nyota hao wa Arsenal
kujitahidi kucheza soka la kuvutia, wakati wa mapumziko, Wenger aliwakoromea
akidai walishindwa kumudu staili hiyo ya uchezaji.
Kocha huyo pia alimpondo Gervinho kwa
kukosa nafasi katika kipindi cha kwanza, lakini yote kwa yote ni wachezaji hao
kubaini mpasuko kati ya Wenger na Bould ambaye alitua 'The Gunners' katika
majira ya joto kuziba nafasi ya Pat Rice.
Chanzo kimoja kilisema: “Kunaonekana
hakuna mawasiliano makubwa kati ya wawili hao. Ni aibu kwa sababu wachezaji
wote wanaonekana kuwa nyuma ya Wenger, ingawa pia mambo ni sawa kwani wote
wanamkubali Bould. Mambo yanatia hofu.”
Chanzo hicho kilieleza kuwa, Wenger
bado ndiye kiongozi mkuu wa wachezaji. Kikaongeza: “Bould anawanoa mabeki kabla
hata ya kuanza kwa msimu, lakini hajawahi kuruhusiwa kufanya maamuzi, Wenger
amekuwa akiamua kila kitu.”
Hilo limewafanya wengi waamini usemi wa
nyota wa zamani wa Arsenal, Stewart Robson, ambaye alimuita Wenger "dikteta".
Hata hivyo, wachezaji hao pia wamemtaka
Wenger kubadili mfumo wa uchezaji wa soka la kuvutia kama Barcelona na kucheza
soka la nguvu na lakushtukiza.
Gazeti la "The Sun",
limeeleza kuwa, wachezaji wa kikosi cha kwanza wameonekana kuwa wanyonge
kutokana na kulazimishwa kucheza soka la kuvutia ambalo mara nyingi linawanyima
fursa ya kupiga mashuti na hata kushindwa kuingia kwenye 18.
Chanzo hicho kilisema: “Arsenal huwa
inacheza soka zuri, lakini haliwezi kuwa na mvuto kama la Barcelona.
“Mbali na hilo, pia wachezaji wanataka
kazi ya kupanga safu ya ulinzi ibaki mikononi mwa Bould, huku pia wakishangaa
kwanini Gervinho anaruhusiwa kucheza kama mshambuliaji wa kati wakati wengine
wakilazimishwa kucheza nafasi zisizo zao.”
No comments:
Post a Comment