Wednesday, October 17, 2012
NCHI TISA ZATHIBITISHA KUSHIRIKI ROCKY CITY MARATHON
JUMLA ya nchi tisa zinatarajiwa kushiriki mbio za kilomita 21 za Rock City Marathon 2012, zinazoandaliwa na Kampuni ya Capital Plus International (CPI).
Mbio hizi zitafanyika Oktoba 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Akizungumza na BINGWA, jijini Dar es Salaam jana, Mratibu wa mbio hizo Grace Sanga, alisema nchi zitakazo shiriki ni Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC), Australia, India, Canada na Marekani, huku akidokeza maandalizi mazuri yamechangia ongezeo la washiriki.
“Tumetuma mialiko ya kushiriki kwa wadau wote wa riadha wa nchi jirani ili wapate kushiriki Rock City Marathon 2012, ndio maana tunategemea kupata washiriki wengi zaidi kutoka nje ya nchi, kulinganisha na mwaka uliopita na maboresho ya mbio hizi yamechangia kuongeza ushindani”, alisema Grace.
Pia aliongeza kuwa, mbio hizo za kila mwaka zimegawanywa katika makundi matano ya mbio za kilomita 21 kwa wanawake na wanaume, kilomita tano kwa watu wote, kilomita tatu kwa walemavu, kilomita tatu kwa wazee kuanzia miaka 55 na kilomita mbili kwa watoto wa kati ya miaka saba hadi kumi.
Mbio zitaanzia kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kupitia njia tofauti na kurudi uwanjani hapo.
Rock City Marathon zilianzishwa mwaka 2009, ambapo mwaka huu ziko chini ya udhamini wa NSSF, Airtel Tanzania, Geita Gold Mine, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), PPF, African Barrick Gold, New Africa Hotel, Nyanza Bottles, New Mwanza Hotel, TANAPA na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
Mbio hizo zinasubiriwa kwa hamu na wakazi wa Kanda ya Ziwa na zitapambwa na burudani ya aina yake kutoka kwa nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini Juma Kassim ‘Sir Nature’.
Aidha, Grace alisema kuwa, pesa zitakazopatikana kutokana na ada ya usajili wa washiriki zitapelekwa katika mfuko wa msaada kwa watu wenye ulemavu waishio jijini Mwanza.
Usajili wa washiriki unafanyika kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, Ofisi za Capital Plus zilizopo jengo la ATC ghorofa ya tatu na kwenye blog ya rockcitymarathon.blogspot.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment