MOROCCO YAFUNGUA AFCON 2025 KWA USHINDI WA 2–0




Morocco imeanza kampeni yake ya kuwania ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kwa ushindi wa mabao 2–0 dhidi ya Comoro, mchezo uliopigwa Jumapili katika Uwanja wa Prince Moulay Abdellah mjini Rabat, na kujihakikishia pointi tatu muhimu katika Kundi A. 

Wenyeji walitawala mchezo huo ambao uligawanyika katika vipindi viwili tofauti; Comoro wakijilinda kwa nguvu kipindi cha kwanza, huku Morocco wakiongeza kasi na ufanisi baada ya mapumziko.

Mchezo huo ulianza mara baada ya sherehe za ufunguzi zilizopambwa na uwepo wa Mwana wa Mfalme, Moulay El Hassan, ambaye pia alizindua mchezo huo rasmi baada ya kuwasalimia wachezaji uwanjani.

Kipindi cha kwanza kilimalizika bila kutingishiana nyavu, huku Comoro wakitumia mfumo wa ulinzi ulioshikamana ambao ulifanikiwa kuzima mashambulizi ya mfululizo ya Simba wa Atlas (Atlas Lions). Morocco walikaribia kupata bao muda mfupi kabla ya mapumziko baada ya Brahim Diaz kuangushwa na kupata penalti, lakini Soufiane Rahimi alishindwa kuifunga baada ya kipa wa Comoro kuucheza mpira huo.

Hata hivyo, Morocco walifanikiwa kuvunja ukuta wa Comoro katika dakika ya 55 kupitia kwa Brahim Diaz aliyeweka mpira wavuni mapema kipindi cha pili. Ayoub El Kaabi alihitimisha ushindi huo kwa mtindo wa aina yake katika dakika ya 74, akifunga bao la pili kwa shuti la sarakasi (overhead kick).

Kutokana na ushindi huo, Morocco inaongoza Kundi A ikiwa na pointi tatu, angalau kwa muda. Mchezo wa pili wa kundi hilo utazikutanisha Mali dhidi ya Zambia siku ya Jumatatu katika dimba la Mohammed V Sports Complex mjini Casablanca.

Maoni baada ya mechi

Stefano Cusin – Comoro: "Tulikuwa imara sana kwenye ulinzi. Lakini katika mchezo wa aina hii, nafasi inapojitokeza, ni lazima uitumie. Timu imeonesha taswira nzuri, na Wacomoro wanaweza kujivunia nchi yao. Hatuwezi kusema tulicheza vibaya kwa sababu tu tumefungwa mabao mawili. Kama Rafiki angalifunga na kufanya matokeo kuwa 1–1, mchezo ungalichukua mkondo tofauti kabisa. Morocco ni timu kubwa; ni lazima tukubali matokeo tunapofungwa na timu ya aina hii."

Walid Regragui – Morocco: "Tumekuwa tukijiandaa kwa mchezo huu kwa mwaka mmoja na nusu. Tulijiongezea shinikizo kubwa sisi wenyewe. Tulianza vibaya; kuanzia penalti tuliyokosa hadi Romain Saïss kulazimika kutoka nje kwa majeraha. Wakati wa mapumziko, sikuwa nimeridhika sana na timu, kwa hiyo tulizungumza ili kufanya marekebisho fulani, na wachezaji walitekeleza maelekezo hayo kwa haraka sana."

Uchambuzi wa Haraka: 

Inaonekana Morocco walikuwa na hofu ya "laana ya mwenyeji" (pressure ya nyumbani), lakini uzoefu wa Regragui kufanya mabadiliko ya kiufundi kipindi cha pili ndio uliokoa jahazi. Kwa upande wa Comoro, wameonesha kuwa hawatakuwa "mnyonge" kwenye kundi hili, jambo ambalo ni onyo kwa Mali na Zambia.

No comments