CAF Yaruhusu Milango Wazi: Mashabiki Kuingia Bure Viwanjani AFCON 2025
Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) limeruhusu mashabiki kuingia bure kwenye viwanja vinavyohodhi mechi teule za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, ambalo kwa sasa linaendelea nchini Morocco. Kwa mujibu wa vyanzo ndani ya shirikisho hilo vilivyokaririwa na shirika moja la habari la kimataifa, hatua hii inalenga kuwasaidia waandaaji kuongeza idadi ya watazamaji kwenye mechi ambazo zina mahudhurio madogo.
Ili kuzingatia taratibu za usalama na udhibiti wa milango, mashabiki wanaruhusiwa kuingia bure takriban dakika 20 baada ya mchezo kuanza.
Ingawa hakukuwa na tangazo rasmi la awali, utaratibu huu ulifanyiwa majaribio wakati wa mechi za kwanza za hatua ya makundi. Jumatatu iliyopita, mchezo kati ya Misri na Zimbabwe (2–1) katika uwanja wa Agadir ulichezwa kwa milango wazi, jambo lililowaruhusu mashabiki na wakazi wa eneo hilo kuingia bure na kujaza majukwaa yaliyokuwa wazi. Siku iliyofuata, mbinu hiyo ilitumika pia kwenye Uwanja wa Al Madina mjini Rabat, ambapo tiketi za bure ziligawiwa kwa ajili ya mchezo kati ya DR Congo na Benin (1–0) kutokana na idadi kubwa ya viti vilivyokuwa wazi.
Mbinu hiyo ilijirudia tena wakati wa mchezo wa Algeria dhidi ya Sudan (3–0) kwenye Uwanja wa Moulay El Hassan mjini Rabat. Siku hiyo hiyo, mtanange kati ya Cameroon na Gabon (1–0) huko Agadir ulianza huku kukiwa na viwanja vitupu, lakini baada ya kuruhusu watu kuingia bure, idadi ya watazamaji ilifikia 35,200 kati ya uwezo wa uwanja wa kuchukua watu 45,000.
Hatua hii inajaribu kutatua changamoto ya muda mrefu inayozikabili nchi zinazoandaa AFCON: namna ya kuhakikisha viwanja vinajaa kwenye mechi za kimataifa na za bara. Mbali na faida za kiufundi kama usimamizi wa umati na ugawaji wa tiketi, hatua hii pia inatoa mbadala wa kuzuia ulanguzi wa tiketi (soko la kiza), huku ikiboresha hali ya msisimko na ushangiliaji ndani ya viwanja.

Post a Comment