TUME HURU YATANGAZA TAKWIMU MPYA ZA WAPIGA KURA, IDADI YAONGEZEKA KWA ASILIMIA 26.53



Na Mwandishi Wetu

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa taarifa kwa umma ikielezea mabadiliko ya takwimu za wapiga kura na vituo vya kupigia kura vitakavyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Mabadiliko hayo yanafuatia Tume hiyo kupokea taarifa rasmi kutoka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Kutokana na uchakataji wa taarifa za wapiga kura wa ZEC kukamilika, idadi ya jumla ya wapiga kura walioandikishwa nchini sasa imebadilika na kufikia 37,647,235 badala ya 37,655,559 iliyotangazwa awali na Tume hiyo tarehe 26 Julai, 2025. 

"Hii inawakilisha ongezeko kubwa la asilimia 26.53 kutoka kwa idadi ya wapiga kura 29,754,699 waliojiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura mwaka 2020" inasema sehemu ya taarifa hiyo kwa vyombo vya habari,ilioyosainiwa na Mkurugenzi wa uchaguzi Ramadhani Kailima.

Katika taarifa hiyo imeoneshwa kuwa wapiga kura 36,650,932 wapo Tanzania Bara, huku Wapiga Kura 996,303 wakiwa Tanzania Zanzibar. 

Kuhusu jinsia, wanawake wanaendelea kuwa wengi katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ambapo wanawake ni 18,950,801 sawa na asilimia 50.34, ilhali wanaume ni 18,696,439 sawa na asilimia 49.66. 

Aidha, idadi ya vituo vya kupigia kura vitakavyotumika ni 99,895 badala ya 99,911 vilivyotangazwa awali,kutokana na marekbisho yaliyofanywa na ZEC. Hata hivyo vituo hivyo ni sawa na ongezeko la asilimia 22.47 ya vituo vilivyotumika mwaka 2020, ambavyo vilikuwa 81,567. 

Katika Vituo hivyo 99,895 , Tanzania Bara itakuwa na vituo 97,348 na Tanzania Zanzibar itakuwa na vituo 2,547.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, uandikishaji wa wapiga kura kwa uchaguzi wa Rais na Wabunge upande wa Tanzania Zanzibar utazingatia sheria inayohusu uandikishaji wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. 

Hivyo, Daftari la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar litakuwa ni sehemu ya Daftari la Wapiga Kura la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Tanzania Zanzibar.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bw. R. K. Kailima, amethibitisha kwamba Tume itavipatia vyama vya siasa vinavyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 orodha kamili ya vituo vya kupigia kura vitakavyotumika katika uchaguzi wa Rais, Wabunge, na Madiwani. 

Wakati wananchi wanahimizwa kwenda kupiga kura,Kauli mbiu ya Tume inahimiza, "KURA YAKO HAKI YAKO JITOKEZE KUPIGA KURA".


No comments