Pages
▼
Tuesday, October 1, 2024
Simba Queens, Yanga Princess hapatoshi
BINGWA mtetezi wa Ngao ya Jamii, Simba Queens kesho inacheza na Yanga Princess katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii kwa soka la wanawake Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Simba Queens walipata ubingwa kwa kuwafunga JKT Queens kwenye mchezo wa fainali Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na mchezo huo unatarajiwa kuwa wa upinzani kwa sababu msimu uliopita Yanga Princess alifungwa na Simba katika michezo yote.
Kocha Msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’ alisema Yanga Princess ni timu nzuri na walipokutana nao msimu uliopita kwenye hatua kama hiyo waliwafunga. Alisema mchezo wa kesho dhidi yao hautakuwa rahisi.
“Yanga Princess ni wazuri na kila msimu wanajipanga na kuimarika kutafuta kile wanachokitaka, msimu uliopita hatua kama hii tuliwafunga kwa penalti na kwenda kuchukua kombe kwa kuwafunga JKT Queens kwenye mchezo wa fainali. Tunaamini utakuwa mchezo mgumu kwa sababu watataka kulipa kisasi,” alisema Mgosi.
Kocha wa Yanga Princess, Edna Lema alisema: “Mchezo utakuwa mgumu kama ilivyo kawaida ya mechi hizi za watani wa jadi, Simba Queens ni timu nzuri na wachezaji wao ni walewale, hivyo tunatarajia mchezo utakuwa mgumu na sisi kwa upande wetu tumejiandaa vizuri kuwakabili,” alisema Lema maarufu kama Mourinho.
Mchezo wa mapema utazikutanisha JKT Queens na Ceasiaa Queens.
Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu michuano ya Ngao ya Jamii itazikutanisha timu nne bingwa wa ligi dhidi ya mshindi wa tatu na mshindi wa pili dhidi ya mshindi wa nne.
Simba Queens ndio bingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2023/2024 iliyoshirikisha timu 10.
No comments:
Post a Comment