Pages

Sunday, August 27, 2023

MAJESTIC THEATRE, JENGO KONGWE LINALOENDELEA KUONESHA SINEMA

 





Na Rahel Pallangyo

WAKATI wa safari yangu ya Tanga hivi karibuni katika michuano ya Ngao ya Jamii kwenda kuandika habari na kupiga picha za michezo, nilipita karibu kabisa na jumba la sinema la Majestic lililopo barabara ya Mkwakwani.

Jumba hilo la Shirika la Nyumba (NHC) ni la zamani na mpaka sasa linaendelea kuonesha filamu na kufanya kazi nyingine za burudani. Ikumbukwe kuwa katika miaka ya 1980 ambako kulikuwa na mdororo wa kiuchumi hamu ya kwenda sinema ilipungua kutokana na majumba hayo kutokuwa na bidhaa mpya inayovutia wakawa wanababia na kuchosha wapenzi wa sinema. Katika jengo hilo Tanga wapenzi wa sinema wanaopenda kuona vitu hivyo katika ‘Big Screen’ walipoteza burudani hiyo kutokana na kufungwa kwa majumba ya sinema ambayo yalikuwa na uwezo wa kuonesha mm 35 bado wanaendelea kuona kwa kutumia jengo lao ambalo ujenzi wake ni urithi safi wenye kumbukumbu. Ingawa wapenzi wa burudani hiyo kabla ya miaka ya 1980 hawakuweza kufikiri hata mara moja kwamba kutakuwa na kufungwa kwa majumba ya sinema ukizingatia wananchi walikuwa wanafurika kuona sinema za kidosi au za kizungu. Mathalani Dar es Salaam majumba yote yaliyokuwa yakionesha filamu kama Drive in, Empire, Avalon, Empress, Odeon, Cameo, New Chox na Star Light yamegeuka kuwa majumba ya kazi nyingine na mpaka kesho inaonekana haiwezekani tena kurejea katika mazingira ya zamani. Ukiachia Dar es Salaam mji wenye starehe za kipekee wa Morogoro ulikuwa na Shani Cinema na Sapna. Vivyo hivyo katika Mkoa wa Lindi ambapo pale penye ukumbi unaoitwa Y2K kulikuwa na jengo kubwa la filamu. Mpaka mwishoni mwa miaka ya 1990 ilikuwa ni ada kutafuta magazeti kuona nini kinaendelea katika majumba ya sinema ya Dar es Salaam na hata huko mikoani katika mbao za matangazo ya majumba hayo. Ingawa majumba mengi yamekuwa nyumba za ibada, maduka au yamefungwa au kubomolewa na majengo mengine kusimamishwa badala yake, Tanga wameonesha kwamba Majestic yao ambayo ilitumika kuonesha filamu ya kwanza huru, Shamba Kubwa, inaweza kuendelea kuwapo. Majestic Theatre haikuwa peke yake katika mji huu ambao kuingia ni rahisi na kutoka ni kazi kwani kulikuwa na Regal, Novelty na Tanga Cinema lakini leo hii unaona kwamba Majestic ndio wameendelea kuwapo mpaka kesho na bado wanaonesha inawezekana kuendelea kuonesha filamu. Historia inasema katika Jiji hilo jengo la kwanza kufa ni Tanga cinema, ikafuata Novelty, Regal na mwisho Majestic ambao kwa sasa wamefufuka. Nilipata nafasi ya kuzungumza na mmoja wa walimu wa sanaa ya filamu, Profesa Martin Mhando kuhusiana na jengo la Tanga na kuniambia ndilo lililotumika kuonesha filamu ya kwanza huru ya Shamba Kubwa ambayo pia ploti yake ilikuwa Mkoa wa Tanga. Aliniambia ingawa Majestic ya Tanga haina uhusiano na jengo la jina kama hilo Zanzibar ambalo lilipiganiwa kuimarishwa na kuendelea na kazi yake ya kuonesha filamu, anaamini utamaduni wa kuona sinema unarejea kutokana na juhudi mbalimbali za watengeneza filamu hapa nchini na duniani kwa ujumla. Shamba Kubwa moja ya filamu zilizoanzisha tena utengenezaji wa filamu Tanzania baada ya kampuni ya filamu kufa na filamu zake kubaki Zimbabwe zilipoenda kwa ‘treatment’. Shamba Kubwa sinema ya mwaka 1994 ilimtambulisha Jimmy Mponda kama J. Plus wengine wakimuita Jimmy Master ilipata jina kubwa na pia kuleta vuguvugu mpya ya matamanio ya burudani kupitia majumba ya sinema. “Majestic Theatre ya Tanga naijua kama moja ya majumba ambayo yalibaki kuonesha filamu kwa muda mrefu wakati majumba mengine yalipokufa kabisa Tanzania. Mwaka 1995 ilipotengenezwa Bongo Movie ya kwanza iliyoitwa “Shamba Kubwa” na Amri Bawji na Kassim El Siagi, filamu hiyo ilioneshwa Majestic, Tanga,” anasema Profesa Mhando na kusema kuwa hali iliyokuta majumba ya sinema nchini Tanzania Bara na Visiwani matokeo ya mdororo wa kiuchumi. “Uchumi ulidorora miaka ya 1980,” Mhando alisema. “Tiketi zilikuwa zimegharimu dola za Marekani 1-2, lakini tulijua ikifika dola 3 uchumi wa sinema utaporomoka na ndivyo ilivyokuwa. Watu hawakuwa na uwezo wa kutazama sinema. Video zilikuja na kukaa ndani. Kufikia 1996, sinema zote zilikuwa zimefungwa.” Anasema ingawa hana uhakika kuwa Majestic ya Tanga na Majestic Zanzibar zilihusiana ingawa inawezekana, maana waliokuwa wanahodhi majumba ya sinema walikuwa Watanzania wenye asili ya India, kuendelea kuwepo kwa jengo hilo likiendelea na kazi ya kuleta burudani inatia matumaini si tu kwa urithi wa kizazi kijacho bali na uhakika wa maeneo ya kuonesha uwezo wa binadamu katika skrini kubwa. Anasema alikuwa anapigania sana Majestic ya Zanzibar na anafikiria safari ni nzuri kwa kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa tayari kulifufua Jumba la Majestic kwa kupata misaada ya kimataifa. “Mimi nimekuwa nikipigia kelele na kuliwekea kifua ili lisibadilishiwe matumizi kama majumba mengine. Kwa sasa jumba hilo limetolewa kwa Muungano wa taasisi tano kusimamia ukarabati na kulipa matumizi mengi zaidi,” anasema Profesa huyo ambaye amebobea katika filamu. Taasisi hizo tano ni ZIFF, Hifadhi, Sauti za Busara, Women Reclaim Center na Abdul Mawazo. Anasema Unesco imesaidia kupata kiasi cha fedha toka serikali ya Japan ili kufanya upembuzi yakinifu na kuanza mipango ya kukarabati jumba hilo. Ingawa kuna utata katika uhodhi/umiliki wa jumba lenyewe maana nalo lilitaifishwa wakati wa mapinduzi na sasa familia iliyokuwa inalimiliki imerudi tena ili kutaka kuliendesha, mazungumzo yanaendelea kuhusu umiliki na hivyo kazi ya upembuzi imesimama. Unesco ndiyo inasimamia ukarabati. Hekaheka za kurejesha jumba hilo la Zanzibar linaenda na ukweli kuwa majumba ya sinema katika miaka ijayo ni muhimu katika kuhakikisha ukuaji mzuri wa tasnia kwani hata Ulaya walikoendelea bado majumba ya sinema yanafanyakazi hasa kuwezesha pato la kwanza katika kuingia katika majukwaa mengine. Majestic ya Zanzibar ni moja ya majumba ya kwanza ya sinema barani Afrika, katika miaka ya 1920. Zanzibar ilikuwa na majengo ya sinema 53 yakajifia na kubaki mawili likiwemo hilo la Majestic. Mtengenezaji wa filamu Mwingereza Nick Broomfield, anayejulikana kwa filamu za Biggie na Tupac, Aileen Wuornos: The Selling of a Serial Killer na Battle For Haditha anafurahishwa na juhudi za kurejeshwa kwa majumba ya sinema. Akizungumzia jumba la Zanzibar ambalo halina paa kwa sasa watu wakiangalia sinema wazi alisema: “Ingawa sinema haina paa, watu wanaitumia na kuweka projekta yao wenyewe. Pengine ina kumbukumbu nyingi kwao. Ni mahali ambapo watu walienda kwa kustarehe na kukutana na rafiki zao wa kike wa kwanza. “Sinema ni uzoefu wa pamoja. Kama mtengenezaji wa filamu, jambo la ajabu zaidi kuhusu kutazama na kikundi cha watu ni kwamba unaweza kujua ni sehemu gani za filamu zinafanya kazi na zipi hazifanyi kazi. “Ni jambo la kuunganisha, njia ya kufanya kikundi au eneo pamoja. Nilipokuwa mdogo, kila mtu alienda kwenye sinema Jumamosi asubuhi ili kuona katuni. Ilikuwa ni ushirikiano wa kijamii, na hiyo ni moja ya mambo ya kusisimua ambayo yanaweza kutokea. “ Broomfield anasema: “The Majestic ni kipande cha usanifu wa ajabu ... Kwa upande wa jumuiya ya watengenezaji filamu wa Afrika Mashariki, umuhimu wa Zanzibar ungewekwa katika kufufua Majestic. Ingekuwa faraja kwa watu kuchukua sinema kwa uzito. Pia itakuwa vyema kwa tamasha la filamu la Kimataifa la Zanzibar.” “Nadhani ikiwa ingerekebishwa ipasavyo, watu wangeweza kwenda kwenye sinema huko mara kwa mara. Bado ina mapambo mazuri ya sanaa.” Mmoja wa wapenzi wa sinema Beda Msimbe anasema ana tumaini kizazi kipya kikionja ladha ya kuingia majumba makubwa na utamaduni wake wataona raha. “Wazee bado wana ndoto zao za kutazama sinema kila wiki, wanakumbuka utukufu wa zamani wa majumba haya na enzi za ujana wao. Huo ndio umuhimu wa utamaduni wa sinema kwao.” Majestic ya Tanga hivi karibuni ilionesha filamu ya kisayansi ya Eonii na mhudumu wa jumba hilo anasema walijaza watu wa rika zote na kutamani hali hiyo kuendelea kuwa hivyo.

No comments:

Post a Comment