Pages

Saturday, February 10, 2018

SIMBA KUTUPA KARATA YAKE YA KWANZA KIMATAIFA KESHO UWANJA WA TAIFA

SIMBA kesho inashuka kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kucheza mechi ya kimataifa kwa mara ya kwanza baada ya miaka takriban mitano.
Vinara hao wa Ligi Kuu Bara, wataikabili Gendarmerie ya Djibouti katika mechi ya hatua ya awali ya michuano ya kombe la Shirikisho Afrika.
Simba inashuka kwenye mchezo huo huku ikiwa na mwendo mzuri kwenye mechi za Ligi Kuu Bara baada ya kucheza mechi 17 ikiwa kileleni mwa msimamo kwa kufikisha pointi 41  bila kufungwa mechi hata moja.
Mchezo huo ni muhimu kwa Simba kuibuka na ushindi ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kusonga mbele hatua inayofuata kwani itatakiwa kucheza mchezo wa marudiano wiki ijayo ugenini. Djibouti.
Akizungumza na gazeti hili, Kocha wa Simba, Pierre Lechantre alisema kuwa mchezo huo ni muhimu kwa upande wao na anachokihitaji ni ushindi.
Alisema kuwa tayari alishazinasa CD za mechi zilizopita za wapinzani hao na kuzifanyia kazi hasa mbinu wanazozitumia, hivyo haitakuwa ngumu kwao kukabiliana nao.
Aliongeza kuwa atafanya kila awezalo kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo kwani anajua wanachohitaji Simba kwa sasa ni ushindi katika kila mechi, hivyo na yeye anataka kuhakikisha anawapa kile wanachokihitaji.
“Nilishapata mbinu zao muda mrefu sana na nilisha zifanyia kazi kuona nakabiliana nao kwa staili ipi, nitahakikisha hawatoki salama kama mechi ni bora nimalize hapa hapa Tanzania hata nikienda kwao tusiwe na wasiwasi kuwa labda watatutoa.

“Nimekuja Simba kwa kazi moja tu ya kuipa mafanikio, hivyo mtihani mwingine ni huu kwenye mechi yangu ya kwanza ya kimataifa na hivyo nahitaji kujenga imani kwa mashabiki wa Simba,” alisema Lechantre.

No comments:

Post a Comment