SIMBA ya Dar
es Salaam kesho inashuka kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kusaka pointi
tatu dhidi ya Kagera Sugar ili kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, baada
ya leo kuondolewa na Azam FC.
Azam FC jana
iliitoa Simba kileleni baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya
Tanzania Prisons katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya
Sokoine, Mbeya.
Simba
walitua salama kwa ndege mjini Bukoba na walifanya mazoezi kwenye
uwanja huo wa Kaitaba wakijiandaa kwa pambano hilo linalotarajia kuwa kali.
Wekundu hao
wa Msimbazi wanashuka dimbani baada ya kuwachapa Singida United kwa mabao
4-0 katika mchezo wa ligi hiyo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam.
Mganda
Emmanuel Okwi baada ya juzi kutupia bao mbili peke yake wakati Simba ikiibuka
na ushindi huo mnono, leo ataendelea kutegemewa na timu yake kutokana na makali
yake.
Simba
inashuka uwanjani leo ikiwa mkononi ina akiba ya pointi 29 baada ya kushuka
dimbani mara 13, ikiwazidi pointi nne mabingwa watetezi Yanga, ambao jana
waliifunga Ruvu Shooting 1-0.
Na sasa
Wekundu wa Msimbazi kwa kuhakikisha wanaendeleza wimbi la ushindi, wamewasili
mapema Bukoba kwa usafiri wa anga ili kufanya maandalizi mazuri.
Timu hiyo
inacheza mchezo wake wa pili tangu kuwasili kwa kocha Mfaransa Pierre Lechantre
aliyewasili wiki iliyopita na kuishuhudia timu hiyo ikiifunga Singida mabao
4-0.
Kocha huyo
tayari ametambulishwa rasmi, lakini haijaelezwa ameingia mkataba wa miaka
mingapi.
Ilielezwa
kuwa kocha huyo Mfaransa ametua Simba kwa ajili ya programu maalumu ya vijana
na ile ya timu ya wakubwa.
Lechantre
ambaye ataanza kazi timu itakaporejea kutoka Bukoba, aliomba apewe angalau
miezi minne ili Simba wafurahie matunda yake.
Kagera Sugar
iko nafasi ya nne kutoka mkiani ikiwa na pointi zake 12 baada ya kushuka
dimbani mara 13, hivyo ni timu dhaifu hadi sasa ukilinganisha na Simba.
No comments:
Post a Comment