Makocha
28 wanawake kutoka vyuo mbalimbali vya Maendeleo ya Jamii nchini leo Oktoba 17,
2017 wamehitimu kozi fupi ya ukocha katika kozi iliyoratibiwa kwa pamoja kati
ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Taasisi ya Karibu Tanzania
(KTO).
Kozi hiyo ya siku mbili ambayo ni ya pili kufanyika kwa makocha
hao, iliyofanyika kwenye Uwanja wa Karume - Makao Makuu ya TFF ilikuwa chini ya
mkufunzi wa TFF, Raymond Gweba.
Akizungumza kwenye ufungaji wa kozi hiyo Mkurugenzi wa Maendeleo
ya Michezo, Yusuph Singo amesema Serikali inafahamu kuwa inatakiwa kuwekeza
kwenye soka la wanawake kuanzia upande wa vijana na ndio maana inatengeneza
mazingira na sera zitakazowezesha mafanikio hayo.
Singo amesema nchi mbalimbali wana maendeleo makubwa katika
mpira wa miguu kwa wanawake na sasa wakati wa Tanzania kuwekeza katika upande
huo kuanzia kwa watoto na makocha.
Kadhalika, Singo amewataka wahitimu kuchukuwa mafunzo hayo kwa
uzito mkubwa kwa sababu mpira wa miguu ya ajira na elimu hiyo itaongeza kitu
kikubwa kwao.
Naye, Mwenyekiti wa Chama Mpira wa la Wanawake (TWFA), Amina
Karuma amesema lengo la chama chake na TFF kuhakikisha soka linachezwa nchi
nzima linaelekea kutimia.
Amewataka wahitimu hao wa kozi hiyo fupi kuvitumia vyeti
walivyovipata kuendeleza soka la wanawake na kufanyia kazi yale yote
waliyofundishwa.
Pia ameiomba Serikali kuwaunga mkono katika maendeleo ya soka la
wanawake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ufundi wa TFF Salum Madadi
amesema kufundisha watoto kuna changamoto nyingi, lakini makocha hao
wamefundishwa maarifa ya jinsi ya kukabiliana nazo.
Amesema maarifa hayo sio makocha wote wanaweza kuyapata lakini
wameona umuhimu mkubwa kwa wahitimu hao kuweza kuyapata ili kwenda kuibua
vipaji kuanzia chini.
Wahitimu wa kozi hiyo wamepatiwa vyeti vya ushiriki na vifaa vya
michezo ikiwemo koni na mipira.
No comments:
Post a Comment