Pages

Thursday, October 19, 2017

WAAMUZI WA SIMBA NA YANGA HADHARANI


MWAMUZI wa Kimataifa, Hery Sasii anatarajiwa kuwa pilato wa mchezo wa Ligi Kuu Bara, raundi ya nane utakaozikutanisha Yanga na Simba Oktoba 28 mwaka huu.
Sasii wa Dar es Salaam ndiye aliyechezesha mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya watani hao uliomalizika kwa Simba kushinda kwa mikwaju ya penalti 5-3.
Mwamuzi huyo atasaidiwa na mwamuzi msaidizi wa kimataifa Soud Lila wa Dar es Salaam na Mohamed Mkono wa Tanga na mezani atakuwepo mwamuzi msaidizi wa kimataifa, Josephat Bulal.
Sasii nje ya uamuzi ni fundi katika kampuni ya Itech Contractors, katika uwekaji wa vioo na kufanya marekebisho (maintenance) katika majengo pia anamiliki duka la vifaa vya ujenzi.
Akizungumza jana, Sasii alisema  amesomea ufundi wa umeme wa majumbani na wa magari lakini pia alisomea kozi ya ufundi wa kupaua majengo lakini hakuimaliza.
“Mimi nafanya biashara ya mbao na ninamiliki kiwanda kidogo cha kuranda mbao na duka la vifaa vya ujenzi lakini nafanya kazi katika kampuni ya Itech Contractors,” alisema Sasii.
Sasii mwamuzi ambaye anamudu vema kupiga filimbi, kusimamia sheria 17 za soka na asiyeyumbishwa na kelele za mashabiki wala wachezaji atasimamiwa na Kamishna Bwire Manyama ambaye ni mwamuzi mstaafu wa kimataifa.
Kwa upande wa waamuzi wasaidizi wote wamechezesha mchezo wa watani hao wa Dar es Salaam mara tatu ambapo Mkono ambaye ni mwalimu wa masomo ya sayansi Shule ya Sekondari Bungu iliyopo Korogwe amechezesha michezo miwili ya ligi na mmoja wa ngao ya jamii.
Lila ambaye ni miongoni mwa waamuzi chipukizi ambao CAF inawafuatilia na  hivi karibuni ametoka Misri katika kozi amezichezesha katika michezo ya ligi.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment