Pages

Tuesday, October 3, 2017

IDRIS SULTAN NA ERNEST NAPOLEON WAPATA DILI LA KUCHEZA FILAMU MAREKANI

Nyota ya aliyekuwa mshiriki wa shindano la Big Brother Africa, Mtanzania Idris Sultan, inaendelea kung’ara  baada ya ‘kupata shavu’ la kushiriki filamu yenye bajeti ya dola za Kimarekani milioni 17 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 38.
Idris pamoja na Mtanzania mwingine Ernest Napoleon, wataungana na mastaa wakubwa  duniani kama Eric Dame, mwigizaji Mmarekani, Gerard Depardieu wa Ufaransa, Thomas Kretschmann wa Ujerumani na wengine wengi kucheza filamu hiyo ya ujambazi wa kimataifa.
Filamu hiyo itakayojulikana kwa jina la ‘The Blue Mauritius’, inahusu majambazi watano wa kimataifa ambao wanasafiri kwenda katika jiji la Cape Town nchini Afrika ya Kusini, kwa ajili ya kuiba vitu mbali mbali vyenye thamani kubwa duniani.
Idris na mwenzake Ernest Napoleon, watasafiri kwenda katika jiji la Cape Town nchini Afrika kusini mapema mwakani kwa ajili ya filamu hii  kubwa kuwahi kuwahusisha Watanzania.
“D Street inayo furaha kubwa kugeukia vipaji vya waigizaji wa Kiafrika kwa kuwaunganisha na waigizaji wa kimataifa kama itakavyokuwa kwa ‘The Blue Mauritius’,” anasema Dexter Davis, Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya D Street Media Group ya Marekani, inayoanda filamu hiyo
Kwa mujibu wa Davis, filamu hiyo itasambazwa siyo tu Marekani, bali pia katika majumba makubwa ya sinema dunia nzima.
“Ernest na Idris watang’ara, tunasubiri kwa hamu kuwaona tena kwenye skrini kubwa wakifanya makubwa,”anasema Davis.
Mapema mwaka huu, wawili hao walicheza filamu iliyojulikana kama ‘Kiumeni’ ambayo pia Ernest alikuwa ni mzalishaji na kushirikiana na Daniel Manege kuiandika. Filamu hiyo ilishinda katika Tamasha la Timataifa la Filamu la Zanzibar ambalo Idris na washiriki wenzake walihudhuria
“Ninayo furaha kubwa kufanya kazi na Idris katika filamu kubwa kama hii ya The Blue Mauritius. Ni mwaka wa pekee kwa mimi kufanikiwa kufanya kazi na D Street. D Street inabadilisha upepo kwa Afrika inapokuja kwenye suala la kutengeneza filamu,” anasema Ernest 
Kwa upande wake Idris anasema, “Nilikutana Dexter Davis kwenye Maonyesho ya Filamu ya Kimataifa ya Zanzibar mwezi Julai na nilifurahishwa na namna ambavyo amevutiwa na vipaji kutoka Afrika. Alivutiwa kufanya kazi na mimi baada ya kuona ushiriki wangu katika filamu ya ‘Ballin; On the Other side of the World’ na miezi miwili baadaye nilishiriki Katina filamu moja ya Kimarekani. Filamu hizi mbili zimenifanya niweze kufanya kazi nchini Marekani jambo ambalo nilitamani sana,” 
Filamu hiyo inatarajia kuanza kuzalishwa mwishoni mwa mwezi wa tatu mwaka ujao (2018). 

No comments:

Post a Comment