Pages

Tuesday, September 19, 2017

TFF YATAKIWA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI

 Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura Septemba 18, 2017 ametembelea Ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala Dar es Salaam.
Wambura ambaye aliongozana na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Bw. Mohammed Kiganja alilakiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Bw. Kidao Wilfred.

Naibu Waziri Anastazia Wambura alifanya mazungumzo na Kidao kwa muda ambako alijifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata ripoti ya utendaji katika mwezi mmoja tangu uongozi mpya wa TFF uingie madarakani.

Baada ya kupata maelezo ya Utendaji kwa Uongozi mpya amepongeza Uongozi mpya kwa kuanza vizuri na ameridhishwa na mipango ya Uongozi mpya katika program za Vijana na Soka la Wanawake.

Pia amepongeza zoezi la Ugawaji wa mipira 100 kwa mikoa yote ya Tanzania na kusema muhimu ni kutumika ilivyokusudiwa. Anaamini mwanzo mzuri wa Rais Wallace Karia ni dalili njema za kuleta maendeleo makubwa katika soka.

Mbali ya kuzungumza na Kaimu Katibu Mkuu, Naibu Waziri Wambura alikuwa shuhuda wa mazoezi ya jioni ya Timu ya Taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Mara baada ya mazoezi hayo, Naibu Waziri Anastazia alikaribishwa kuzungumza na vijana wa Serengeti Boys, ambako awali kabisa alitaka vijana hao ambao wengi wao wana umri wa chini ya miaka 15 kwa sasa kuwa ni wenye thamani.

“Mtakumbuka kamba Umitashumta mlikuwa wengi, ila mmebaki ninyi. Nataka mjue kuwa Serikali iko hapa na tunafuatilia. Tunataka matunda kutoka kwenu,” alisema Naibu Waziri, huku akiwapa salamu za Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.

Akaongeza: “Nawapongeza sana kwa kuonesha mnaweza. Ila fanyeni mazoezi kwa juhudi, chezeni mpira kwa uhodari, ila msisahau kuzingatia pia masoma. msifanye masihara hata kidogo. Mkizingatia masomo na kucheza mpira, mtafanya makubwa zaidi.

“Naamini baada ya kambi hii mtakuwa vizuri. Je, kwenye mashindano yajayo mtashika namba gani?” alihoji Naibu Waziri Wambura kabla ya vijana kwa pamoja kujibu: “Namba moja.”
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), liliiteua Tanzania kuandaa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 mwaka 2019. Tayari Tanzania imeanza kuandaa timu.

No comments:

Post a Comment