Pages

Sunday, September 17, 2017

OKWI APIGA MBILI SIMBA IKIIFUNGA MWADUI FC 3-0

SeeBait
EMMANUEL Okwi ameendelea kuonyesha kuwa ni moto wa kuotea mbali baada ya kuifungia Simba mabao mawili ‘wakiifukia’ migodi ya Mwadui FC kwa kuitandika mabao 3-0 katika mchezo wa ligi kuu uliofanyika kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Mabao hayo yanamfanya raia huyo wa Uganda kufikisha mabao sita baada ya kucheza mechi mbili na kuwa kinara wa ufungaji katika msimamo hadi sasa.
Okwi alifunga mabao hayo katika kila kipindi ambapo la kwanza alifunga dakika ya saba wakati la pili akifunga dakika ya 57 kwa shuti kali la mguu wa kushoto lililomshinda mlinda mlango Arnold Masawe.
Simba waliendelea kuliandama lango la Mwadui ambapo dakika ya 26 walifanya shambulizi kali na shuti la Shiza Kichuya likigonga mwamba na kutoka nje.
Emmanuel Okwi (kulia) akishangilia bao na John Bocco ‘Adebayor’
Mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’ alimalizia karamu ya mabao kwa Simba kufuatia kufunga la tatu dakika ya 62 kwa kuwahadaa mabeki wa Mwadui na kupiga mpira kwa mtindo wa ‘kuchop’ na kumuacha mlinda mlango Masawe akiwa hana la kufanya.
Kocha wa Simba Joseph Omog aliwapumzisha Nicholas Gyan, Mzamiru Yassin na Kichuya na kuwaingiza Mwinyi Kazimoto, Laudit Mavugo na Jonas Mkude huku Mwadui ikimuingiza Awesu Ally kuchukua nafasi ya Hassan Kabunda.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi baada ya kufikisha pointi saba katika mechi tatu walizoshuka dimbani.
Katika mchezo mwingine wa ligi kuu leo Mbeya City wamefanikiwa kupata ushindi wa pili baada ya kuitungua Njombe Mji bao 1-0 likiwekwa nyavuni na Eliud Ambokile.
 Kwa hisani ya Boiplus blog

No comments:

Post a Comment