Pages

Thursday, September 28, 2017

MWAMUZI APEWA ONYO, RUFAA YA RUVU SHOOTING DHIDI YA KAGERA YATUPWA NA RHINO RANGERS YATOZWA FAINI

Kamati ya Bodi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, iliyoketi hivi karibuni imepitia taarifa mbalimbali ya michezo iliyofanyika ya Ligi Kuu ya Vodacom na Ligi Daraja la Kwanza na kufikia uamuzi ufuatao.
Kamati hiyo maarufu kwa jina la Kamati ya Saa 72, imepitia mchezo namba 18 (Majimaji v Yanga).

Katika mchezo huo Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Bw. Hassan Uhako kutoka Arusha hakuwa makini, hivyo kutomuona mchezaji wa Majimaji, Juma Salamba jezi namba 12 aliyempiga kiwiko mchezaji Emmanuel Martin wa Yanga na kumsababishia maumivu hadi kupoteza fahamu.

Kutokana na kitendo hicho Kamati imeelekeza Mwamuzi Msaidizi huyo ameandikiwa barua ya Onyo Kali kwa kukosa umakini. Adhabu hiyo dhidi ya Mwamuzi huyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 38(5) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.

Pia mchezaji Salamba wa Majimaji kutokana na kumpiga mwenzake kiwiko amesimamishwa na suala lake linapelekwa Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu. Uamuzi wa kumsimamisha umezingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu.

Mechi namba 22 (Stand United v Singida United).

Kocha wa timu ya Singida United, Hans van der Pluijm amepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuingia katika vyumba vya wachezaji na kutoa maelekezo wakati akiwa anatumikia adhabu ya kukosa mechi tatu aliyopata msimu uliopita akiwa na timu ya Yanga.

Adhabu dhidi ya Kocha Pluijm imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 40(13) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha.

Mmiliki wa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga ameandikiwa barua kwa uwanja huo kukosa maji ya bomba na badala yake kutumia maji ya kwenye ndoo au madumu hali hiyo ambayo inahatarisha afya za wachezaji.

LIGI DARAJA LA KWANZA

Mechi namba 2 Kundi A (Mvuvumwa v African Lyon). Timu ya Mvuvumwa FC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi na kuhudhuria wakiwa pungufu. Pia timu hiyo ilichelewa kufika uwanjani ambapo ilifika saa 9.20 mchana badala ya saa 9.00 mchana.

Adhabu dhidi ya Mvuvumwa FC imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza. Kwa kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi, uwanjani na kuhudhuria kikao wakiwa pungufu ni ukiukaji wa Kanuni za 14(2a) na 14(9) za Ligi Daraja la Kwanza.

Mechi namba 1 Kundi B (Mlale JKT v Polisi Tanzania).

Timu JKT Mlale imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kosa la kuchelewa kufika uwanjani. Iliingia saa 9:20 mchana badala ya saa 9:00 mchana. Kitendo hicho ni uvunjifu wa Kanuni ya 14(9) ya Ligi Daraja la Kwanza, na adhabu dhidi yao ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49).

Mechi namba 2 Kundi C (Rhino Rangers v Alliance).

Timu ya Alliance imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kutoingia vyumbani wakati wa ukaguzi na wakati wa mapumziko, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(13) ya Ligi Daraja la Kwanza, na adhabu imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Pia viongozi wa benchi la ufundi la Alliance, Kocha Msaidizi Kessy Mziray, Kocha wa makipa Tade Hussein, Mtunza vifaa Josephat Munge na Meneja wa timu James Bwire wamepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kila mmoja kwa kosa la kumbughudhi mwamuzi wakimtaka kumaliza mpira kabla ya muda wakidai muda umekwisha wakati kazi ya kutunza muda si yao. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41(2) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Rhino Rangers imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) na barua ya Onyo kutokana na mashabiki wa timu hiyo kufanya fujo baada ya mechi kumalizika. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Mechi namba 3 Kundi C (Biashara Utd Mara v Toto Africans). Msimamizi wa Kituo ameandikiwa barua kuelezwa juu ya upotevu wa muda unaofanywa na waokota mipira (ball boyz).

Ball Boyz hao wamelalamikiwa katika mechi hiyo iliyochezwa Septemba 17, 2017 kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma, hivyo ni vizuri wakafahamishwa kuwa kuokota mipira kwa haraka ndiyo wajibu wao unaowafanya wawepo uwanjani.

Mechi namba 4 Kundi C (Dodoma FC v Pamba). Meneja wa timu ya Pamba FC, Salmin Kamau amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mwezi mmoja kwa kosa la kutoa lugha chafu kwa mwamuzi. Adhabu dhidi yake imezingatia Kanuni ya 41(2) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Viongozi.

AJENDA 13/MSC/2017- MALALAMIKO YA RUVU SHOOTING
Kamati imetupa malalamiko ya klabu ya Ruvu Shooting dhidi ya Adeyum S. Ahmed kupinga mchezaji huyo kuichezea Kagera Sugar bila kuwa na barua ya kumruhusu (release letter) kutoka klabu ya Stand United.

Malalamiko hayo yametupwa baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF kueleza kuwa Adeyum ni mchezaji halali wa Kagera Sugar, kwani wakati anasajiliwa na timu hiyo alikuwa mchezaji huru kwa vile mkataba wake na Stand United ulishavunjika, hivyo kutohitaji release letter wakati anajiunga na Kagera Sugar.

No comments:

Post a Comment