SIMBU AANZA KURUDISHA HESHIMA YA RIADHA TANZANIA
MWANARIADHA Alphonce Simbu ameitoa Tanzania
kimasomaso kwenye michuano ya riadha ya dunia ya London Marathon baada ya
kushika nafasi ya tatu.
Kwa mujibu wa habari kwenye mitandao mbalimbali ya kimataifa jana,
mwanariadha huyo amejishindia medali ya Shaba baada ya kushika kwake nafasi
hiyo ambapo alionesha umahiri mkubwa katika kufukuza upepo kwenye mashindano
hayo.
Nusura ashike nafasi ya pili iliyochukuliwa na mwanariadha Tamirat Tola
wa Ethiopia, kwani mkongwe huyo wa Ethiopia alimshinda Simbu kwa sekunde mbili
tu.
Simbu ameshika nafasi ya tatu baada ya kumaliza kwa muda wa saa 2: 09:51
huku mshindi wa kwanza ambaye ni Mkenya, Geofrey Kirui akishinda kwa saa 2:08:
22.
Simbu amemshinda Muingereza Callum Hawkins aliyeshika nafasi ya 4 kwa
kumaliza kwa aaa 2:10:17, huku Gideon
Kipkater raia wa Kenya akishika nafasi ya 5 kwa kumaliza kwa saa 2: 10: 56.
Simbu, mwenyeji wa Arusha na kiongozi wa timu ya riadha iliyoshiriki
michuano hiyo, amewakilisha vema kwa kushika nafasi hiyo ambayo hakuna
Mtanzania aliyewahi kushinda kwenye michuano hiyo.
Simbu alishika nafasi ya tano kwenye michezo ya Olimpiki Rio de Janeiro,
Brazil mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu alishika nafasi ya kwanza kwenye
Mumbay Marathon.
Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania, Filbert Bayi
alimpongeza mwanariadha huyo na kusema hatua hiyo imetokana na maandalizi
mazuri.
Alisema, kitendo cha mwanariadha huyo kupewa Sh milioni 1 kila mwezi na
DSTv ni mchango mkubwa kwake na kwamba kuajiriwa kwake na Jeshi la Kujenga
Taifa, JKT, pia kumesaidia kumwezesha
kufanya vema kwa kuwa imempunguzia mawazo ya kifamilia.
Bayi alikiri kuwa michuano hii aliyoshiriki Simbu ni mikubwa iliyojaa
kila aina ya ushindani na kuwapongeza washiriki wote kutokea Tanzania.
Katika mashindano hayo aliyeshika nafasi ya 6 ni Daniel Meucci kutoka
Italia, huku Yohana Ghebregergis kutoka Eritrea akishika nafasi ya saba. Aliyeshika nafasi ya nane ni Daniel Wonjin
kutoka Kenya.
No comments:
Post a Comment