Pages

Wednesday, August 23, 2017

SIMBA BINGWA WA NGAO YA JAMII










Simba imeanza vyema msimu mpya wa Ligi Kuu ya soka Tanzania bara kwa kutwaa Ngao ya Jamii kwa kuichapa Yanga kwa penalti 5-4 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Alikuwa mshambuliaji Mohammed Ibrahim Mo aliyeamsha shangwe, vifijo na nderemo za mashabiki wa Simba  kwa bao la ushindi.

 Mo alifunga penalti ya tano kwa Simba na kuhitimisha upigaji penalti ulioiacha Yanga ikiishia kupata penalti nne.

 Pamoja na kuanza kupiga penalti huku Simba ikimalizia, Yanga ilikosa fursa ya kubeba ngao hiyo baada ya mshambualiji wao, Mahadhi kukosa penalti ya sita kabla ya Mo kufunga.

Hatua ya kupigiana penalti ilikuja baada ya timu hizo kucheza dakika 90 za kawaida na kutoka suluhu, licha ya kosa kosa kadhaa kila upande.
Ushindi huo wa Simba umeifanya itwae kwa mara ya pili Ngao ya Jamii. Kinara ni Yanga mwenye ngao nne za jamii na Azam moja.

Kabla ya Mo kufunga penalti ya mwisho, Mahadhi alikosa kwa Yanga na kumaliza matumaini ya Yanga kuweka historia nyingine.

Wengine waliopata penalti hizo kwa upande wa Simba ni Method Mwanjali, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima na  Shiza Kichuya.

Mohammed Hussein 'Tshabalala' ndiye peke yake alikosa penalti kwa Simba baada ya kipa wa Yanga, Youthe Rostand kupangua shuti lake.

Kwa upande wa Yanga, Kelvin Yondani na Juma Mahadhi walikosa. Shuti la Yondani lilidakwa na kipa Aishi Manula huku Mahadhi akipaisha mpira kutokana na wasiwasi wake.

Waliopata penalti kwa Yanga ni Kabamba Tshitshimbi, Thaban Kamusoko, Ibrahim Ajibu na Donald Ngoma.
Timu hizo ziliendelea kupigiana penalti zaidi baada ya kipa wa Yanga kupangua penalti ya Tshabalala na kufufua matumaini ya kushinda lakini bila mafanikio.

Awali katika muda wa kawaida, timu zote zilicheza kwa spidi huku zikishambuliana kwa zamu.
 Kivutio kikubwa kwa mashabiki wa Yanga alikuwa Tshitshimbi ambaye alicheza mechi yake ya kwanza Yanga tangu asajiliwe akitokea Mbabane Swallows ya Swaziland.

Ubora na kiwango alichoonesha kiliwakosha mashabiki wa Yanga na kufanya muda wote wamsifu kwa nyimbo kutokana na kuokoa mipira mingi ya hatari langoni mwa Yanga.

Timu zote zilitengeneza nafasi kadhaa za kufunga ndani ya dakika 90 bila mafanikio kutokana  na wafungaji kutokuwa makini.

Waliotengeneza nafasi nzuri za kufunga ni Mavugo, Niyonzima, Luizio na Okwi kwa upande wa Simba. Upande wa Yanga ni Ajibu,  Tshitshimbi, Martin na Kamusoko.

Yanga ilifanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji hasa kipindi cha pili kwa kuwatoa Raphael Daud, Juma Abdul na kuwaingiza Juma Mahadhi na Hassan Kessy, lakini haikuwasaidia.

Simba iliwatoa Laudit Mavugo, Mzamiru Yasini na Erasto Nyoni na kuwaingiza Juma  Luizio, Mohamed Ibrahim na Mohamed Hussein lakini mabadiliko hayo hayakuisaidia kufunga mabao.

Ilibidi Simba isubiri hadi katika upigaji penalti kuwapa furaha mashabiki  kwa ushindi huo.
Mechi ya Ngao ya Jamii inatumika kufungua pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya soka Tanzania bara inayoanza keshokutwa.

Mechi hiyo hukutanisha bingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita ambao ni Yanga na mshindi wa Kombe la FA msimu uliopita ambao ni Simba.

Kikosi cha Yanga: Youthe Rostand, Kelvin Yondani, Vincent Endrew, Juma Abduli, Gadiel Michael, Raphael Daud, Papy Tshishimbi Kabamba, Thaban Kamusoko, Emanuel Martin, Ibrahim Ajibu na Donald Ngoma.

Kikosi cha Simba: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Ally Shomari, Method Mwanjale, Salim Mbonde, Mzamiru Yasini, Haruna Niyonzima, James Kotei, Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya na Laudit Mavugo.

No comments:

Post a Comment