Pages

Sunday, August 27, 2017

LIPULI YAIDUWAZA YANGA UWANJA WA UHURU LEO BAADA YA SARE






MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu bara, Yanga leo imeduwazwa na Lipuli baada ya  kulazimishwa sare ya bao 1-1 katika mechi yake ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Matokeo hayo hayakutarajiwa na wengi kutokana na ugeni wa Lipuli kwenye ligi na hivyo iliingia uwanjani ikiwa haipewi nafasi ya kushinda.
Lipuli iliyopanda Ligi Kuu msimu huu, ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 45 kupitia kwa Seif Abdallah akiunganisha pasi ya Malimi Busungu kabla ya kuachia shuti lililojaa wavuni.
Dakika tatu za nyongeza ziliitosha Yanga kusawazisha bao hilo kupitia kwa Donald Ngoma aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kona wa Thaban Kamusoko.
Mwanzoni mwa kipindi cha pili nusura Busungu aifungie Lipuli bao lakini mpira wa kichwa aliopiga akiwa kwenye nafasi nzuri, ukapaa na kutoka nje.
Dakika ya 76, Kamusoko alikosa bao la wazi, akiwa yeye na kipa wa Lipuli, lakini kipa huyo Agathon Mkwano aliudaka mpira.
Katika mechi hiyo, Lipuli inayonolewa na mchezaji na kocha wa zamani wa Simba, Selemani Matola, ilianza mchezo kwa kasi na kutawala katika kipindi cha kwanza ambapo katika dakika ya 21 ilifanya shambulizi kupitia kwa mshambuliaji wake Abdallah, lakini mpira wake wa kichwa haukulenga lango la Yanga.
Dakika sita baadaye, Ngoma aliikosesha Yanga bao akiwa kwenye nafasi nzuri lakini alipiga vibaya mpira wa kichwa na kutoka nje.
Yanga imecheza mechi hiyo ikitoka kufungwa kwa penalti 5-4 na mtani wake, Simba wiki iliyopita katika mechi ya Ngao ya Jamii kuashiria kuanza kwa msimu mpya wa ligi.
 

No comments:

Post a Comment