“NINAISHI
Marekani lakini mimi ni Mtanzania,” ni maneno ya mshindi wa tuzo tano za
kutunisha misuli, Nelson Issangya ambaye anafanya shughuli zake nchini
Marekani.
Issangya
ambaye ni mtaalamu wa teknolojia ya mawasiliano (IT) anasema amezaliwa mkoa wa
Arusha, wilaya ya Arumeru katika kijiji cha Sakila.
Issangya
anasema alikwenda Marekani mwaka 2003 kusoma shahada ya Computer and
Information Systems na baada ya kuhitimu alipata kazi ya Teknolojia ya
Mawasiliano (IT) huko huko Marekani.
“Baada ya
kwenda Marekani mwaka 2003 nilijiunga na chuo ambapo nilitunukiwa shahada yangu
ya Computer and Information Systems,” anasema Issangya.
Kijana huyo
ambaye ni mpole huku akiongea taratibu anasema alivutiwa na mchezo wa kutunisha
misuli na kuamua kujifunza na kujikuta akifanya vizuri.
“Mbali na
kushindana kwenye mashindano ya kutunisha misuli, ninafanya kazi kama mtaalamu wa mawasiliano, hivyo
mchezo huu naufanya baada ya kazi,” anasema Issangya.
Kwa sasa
ameshajinyakulia tuzo tano katika mashindano mbalimbali aliyoshiriki na kusema
kila shindano analoshiriki anajitambulisha kuwa ni Mtanzania.
“Marekani
ninaishi katika jimbo la Oregon tangu nimewasili na mazoezi nimeanza kufanya toka
nilipowasili wakati nasoma. Mwaka 2015 ndio
nilianza kushiriki mashindano mbalimbali ya kutunisha misuli,“ anasema.
Issangya
anasema ameshinda tuzo mbili za mashindano ya Jimbo la Oregon State, Cascadian
Classic katika Jimbo la Oregon na tuzo mbili za Emerald Cup, katika Jimbo la Washington
State.
Anasema
changamoto anazokutana nazo katika mchezo huu ni jinsi ya kugawa muda wake wa
mazoezi na kazi yake ambayo ni ya kuajiriwa.
“Mimi ni
mwajiriwa na kufanya mazoezi ili kushindana ni changamoto inayonikabili katika
mchezo huu, lakini najitahidi kufanya mazoezi ya nguvu katika muda kidogo
ninaopata,” anasema.
Anasema
malengo yake katika mchezo huu ni kujifunza kadri awezavyo baadae aweze kuwa kocha au mkufunzi
atakaporejea nchini Tanzania.
“Ninataka kujifunza
kadri niwezavyo kwani baadaye nitapenda sana kuelimisha watu hasa Tanzania
jinsi ya kufanya mazoezi na kula vizuri ili kujenga misuli,” anasema.
Issangya
anasema hajulikani na Chama cha Watunisha Misuli cha Tanzania wala kikundi
chochote kinachofanya mchezo huo, licha
ya yeye kujitambulisha katika mashindano yote kuwa ni Mtanzania.
“Napenda
Watanzania wafahamu kuwa kuna kijana wao anaitwa Nelson Issangya anayewatangaza
kupitia mchezo huu hivyo kama kuna Chama cha Watunisha misuli Tanzania
ningependa kuonana nao,” anasema.
Pia kupitia
makala haya anaowamba wale wanaopenda mchezo huu wawasiliane kupitia ukurasa
wake wa facebook wa Nelson Issangya.
Anasema
anatamani siku moja Tanzania iwe na mashindano mengi kama ilivyo Marekani,
ambapo mashindano yapo ya kila aina na kila jimbo hali inayomfanya mshiriki
kuchagua sehemu anayotaka kushiriki.
Issangya
alipata elimu ya msingi katika shule ya Sakila na baada ya kuhitimu alijiunga na kidato cha
kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari ya Makumira.
Baadae alisoma
ufundi katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) cha Dar es Salaam, baada ya kuhitimu
elimu ya ufundi alirudi Arusha na kusoma kozi ya kiingereza na Tour Guide katika
Chuo cha Mount Meru.
No comments:
Post a Comment