SERIKALI
imesema kuna kila sababu kwa Klabu za Tanzania kujifunza mbinu, nidhamu na mafanikio ya
klabu ya Everton ya Ligi Kuu
England mara itakapokuja nchini mwezi
ujao.
Everton na
baadhi ya mashabiki wake inatarajia kufanya ziara nchini ambapo Julai 13, mwaka
huu itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya bingwa atakayepatikana katika michuano
ya Kombe la Sportpesa.
Akizungumzia
ziara hiyo jana kwenye utambulisho wa
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Everton Robert Elston, Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe alisema ujio wa timu hiyo kongwe yenye
umri wa miaka 140, ni fursa kwa klabu mbalimbali kuona na kujifunza namna ya kuendelea.
“Nimepokea
kwa furaha kubwa ujio wa Everton
nikiamini utatusaidia kujifunza badala ya kupigana ngumi kila siku. Klabu,
wachezaji na hata viongozi kwa pamoja wajifunze wafanye nini kuendeleza soka la
Tanzania, ufahari uwekwe pembeni,”alisema.
Dk. Mwakyembe alisema tayari mgeni wao Elston
ametazama uwanja wa Taifa utakaotumika kwa mchezo wa Everton dhidi ya bingwa wa
Sportpesa na kusema hakina tatizo kubwa zaidi kinahitaji kubadilishwa nyasi kwa
kuwa zilizopo zimekaa kwa muda mrefu.
Mbali na
kutarajiwa kucheza Soka Waziri huyo alihimiza klabu hiyo ya kimataifa
kutembelea vivutio vya Tanzania ikiwemo Mlima Kilimanjaro na mbuga za wanyama.
Kwa upande
wake, Elston aliyeongozana na mchezaji wa zamani wa klabu hiyo Leon Osman
alisema timu ya kwanza ya England kuja kucheza Tanzania itakuwa ni sehemu
muhimu ya maandalizi ya msimu mpya ujao.
“Tunafuraha
kuja Tanzania, tunafungua milango mipya, hatuna shaka kwamba tutapa marafiki na
kuongeza mashabiki wetu kimataifa,”alisema.
Alisema
Kocha wao Ronald Koeman na wachezaji wanajiandaa kuja kucheza mechi nzuri dhidi
ya moja ya klabu bora Afrika Mashariki.
Mkurugenzi
wa Utawala wa Sportpesa Abbas Tarimba alisema ziara hiyo iliyoko chini ya
Kampuni hiyo ya bahati nasibu itafanyika sambamba na kutoa elimu kwa makocha na
viongozi wa soka nchini.
Michuano ya
sportpesa inatarajiwa kuanza wiki ijayo ikishirikisha timu nane za Tanzania na
Kenya ambapo bingwa mmoja atacheza na Everton.
Timu
zitakazocheza ni Yanga, Simba, Singida United na Jang’ombe zote za
Tanzania, Tusker, Gor Mahia, Nakuru All
Stars na AFC Leopards za Kenya.
No comments:
Post a Comment