BARCELONA
hawakuweza kukimbizana ipasavyo na Real Madrid msimu uliomalizika wa Ligi Kuu
ya Hispania – La Liga, wakazimaliza mbio wakiwa katika nafasi ya pili nyuma ya
mahasimu wao hao.
Wana
Katalunya wakashindwa kulitetea taji lao kwa tofauti ya alama tatu tu, na laiti
wangezifikisha na kufungana na Los Blancos hao, wangekuwa mabingwa kwa sababu
ya idadi kubwa ya mabao ya kufungwa na machache ya kufungwa waliyo nayo.
Haikuwezekana,
kilichopatikana ni nafasi ya pili, na wameichukua, lakini katika msimu mzima si
kwamba wametoka kapa; kocha Luis Enrique anaondoka akiwa amewapa Super Copa ya
Hispania na Copa del Rey – Kombe la Mfalme na sasa anakwenda kupumzika na
kujitafakari.
Si siri,
umekuwa msimu wenye mambo mengi, mvuto na msisimko kwenye matukio yaliyohusisha
vijana hao wa Camp Nou na yapo mengi yatakayoangaliwa katika historia kwa msimu
huu wa 2016/17 wanaoupa mgongo.
Kuna
wachezaji waliokuwa wapya, waliojiongeza kwenye msimu huu ikilinganishwa na
walivyokuwa kabla, lakini kuna waliochanua hasa na wale waliotokea kuwa
magarasa tu na watatakiwa ama wakubali kukaa benchi au watafute timu nyingine.
Golikipa wa
Barcelona, Marc-Andre ter Stegen alitoka kwenye nafasi ya kuwa kipa msaidizi
hadi kushika namba moja hapo; kwa ujumla alifanya mambo mazuri msimu huu,
japokuwa kwenye mechi nyingine, tena zilizodhaniwa zingekuwa na ushindani mdogo
kwa Barca, hakuwa kwenye kiwango cha juu na Barca wakapoteza pointi kadhaa
zisizokuwa za lazima.
Kadiri muda
unavyokwenda anarekebisha makosa yake na hapana shaka atakuwa mzuri zaidi msimu
ujao, ambapo mtindo wake wa kucheza pia unalandana vyema na wa timu.
Mchezaji
aliyeonesha kipaji binafsi na kujituma zaidi hata kama timu ilikuwa
imegawanyika au kushindwa kushikiwa pamoja ni Lionel Messi. Uwezo wake,
kujituma na kutokata tama vinamfanya kuwa aliyejipeleka uzuri zaidi mchezoni.
Messi
amefunga mabao mengi na mazuri, lakini tunapokuja kwenye bao tamu zaidi la
msimu kutoka kwa watu hawa, naona ni lile la Rafinha, akitundika mpira kwenye
kona ya juu ya goli dhidi ya Leganes, na hii ilikuwa mapema mwanzo wa msimu.
Ukitaka
kuona jinsi Barca walivyojitahidi msimu huu, angalia kwenye Ligi ya Mabingwa
Ulaya (UCL), walivyoweza kupindua kuwa nyuma kwa idadi kubwa ya mabao dhidi ya
Paris Saint-Germain (PSG) wakaja kufuzu kwa nusu fainali walikoadhibika.
Alikuwa
Sergi Roberto aliyefunga bao la mwisho na lililogeuza matokeo na kuwa 6-1 hapo
Camp Nou hata kama baadhi ya watu walilalamika kwamba Barca walipendelewa.
Unaweza kupendelewa lakini ukashindwa kutumia hata fursa hizo. Roberto ni
mchezaji mzuri na wa kuangaliwa siku zijazo.
Ukweli
ukisemwa, ni kwamba kuna wachezaji kadhaa wa Barca wasioonesha kuwa na ufanisi
kiufundi, lakini inawezekana kwamba nyota wa klabu hiyo wanamulikwa mno zaidi,
hata wakasifiwa kwa mabao wanayofunga kumbe yanatokana na jitihada za hawa
wengine.
Watatu ndio
wamekuwa wakitajwa zaidi, katika Messi, Neymar na Luis Suarez lakini kuna
viungo, mabeki na kipa ambao wanaifanya kazi, ndiyo maana hawajafungwa mabao
mengi na wanawazidi Real kwa njia chanya katika uwiano wa mabao ya kufunga na
kufungwa.
Rafinha ni
mmoja wa wachezaji wasioonwa vya kutosha na hao waeneza habari; amekuwa na
msimu mzuri wa kwanza kiungo huyu wa Brazil; anafanya kazi kwa kiwango kikubwa
ikiwa ni pamoja na kuipata mipira, kutoa pasi kwa usahihi lakini pia kufunga
mabao muhimu.
Msimu ule wa
kiangazi Barca walitumia kiasi kikubwa cha fedha kujiimarisha kwenye usajili na
kulikuwapo wachezaji kadhaa waliokuwa na msimu wa kwanza, kama beki wa kati,
Samuel Umtiti, kinda huyu akionesha uwezo wake kiufundi lakini pia kifiziki.
Bado tutarajie mengi na makubwa kutoka kwa Umtiti anayeonekana kujihisi
Barcelona ni nyumbani, akifurahia.
Kwa upande
mwingine wa kipimio kuna mtu anaitwa Andre Gomes ambaye kama ni msimu mbaya
kwake ni huu, tena baada ya kusajiliwa kwa pesa ndefu kutoka Valencia. Amekuwa
akipewa nafasi lakini anachokifanya ni kupoozesha mpira mara kwa mara na
kudhaifisha timu, ikizingatiwa kwamba Enrique amekuwa akitaka mpira uwafikie
pacha wale watatu niliowataja kule mbele mapema iwezekabavyo.
Haikuwa,
hadi wiki za mwisho alipoanza kuipandisha mipira hiyo, lakini tayari Barca
walishajeruhiwa na majaliwa ya ubingwa hayakuwa tena mikononi mwao. Kiulinzi
pia Gomes ni dhaifu, akionekana kuwa sayari tofauti kabisa na Sergio Busquets.
Kuna
wachezaji kadhaa wa Barca ambao wapo kwa mkopo kwenye klabu nyingine, na Munir
ni mmoja wao – akiwa amefanya kazi kubwa sana akiwa na Valencia – akifunga
mabao manane akiwa ni winga. Aliwasaidia kwa sababu jamaa hao wanaojulikana
kama Los Che walikuwa katika hali mbaya kwa muda mwingi wa mwaka, kama si miaka
michache iliyopita.
Kwingineko
kuna mtu anayeitwaCristian Tello aliyekuwa na kawaida ya kuchezeshwa na kufanya
vyema akiwa na Fiorentina wakati Douglas alicheza muda mwingi wa msimu akiwa na
Sporting Gijon walioshushwa. Si yeye aliyesababisha washuke, bali alikuwa mmoja
wa waliojitahidi kuwanusuru. Ni kusubiri kuona iwapo wachezaji hawa
watarejeshwa nyumbani, watabaki huko kwa mkopo au watauzwa kimoja.
Vipi kuhusu
wachezaji ambao mikataba yao inaelekea ukingoni katika kipindi cha miezi 14
hivi ijayo? Wapo na Messi ni mmoja wao. Ni wazi kwamba kwa kazi anayofanya,
Messi anastahili kupewa dili jipya la mkataba na matarajio ni kwamba atausaini.
Mwingine ni
kijana mwenye umri wa miaka 19, Carles Alena, aliyeingia kikosi cha kwanza
msimu huu, akianzia kwenye benchi mechi zaidi ya 10 za La Liga na kuingia mara
kadhaa, kisha akafunga bao kwa mara ya kwanza akiwa na wakubwa wakati wa mechi
ya Copa del Rey.
Kiungo huyu
anacheza soka ya moja kwa moja, miguu yake ni myepesi na anaifanya kazi haraka
na mzuri katika kumaizi pasi – vitu ambavyo Barca wanajitaji na muhimu kutunza
hazina kama hiyo. Aprili ilidaiwa kwamba angesainishwa mkataba mpya, lakini
bado hakuna taarifa rasmi juu yake.
Kwa ujumla
ni sahihi kusema kwamba kikosi cha kwanza cha Barca msimu huu kimekuwa ni timu
inayopata matokeo mazuri lakini wakati mwingine pia kikiishia kutibuliwa – na
ni moja ya maeneo madogo madogo waliyokwama msimu huu na ukweli ni kwamba
hawana wachezaji wengi wa kuziba mapengo, tofauti na Real Madrid.
Hata hivyo,
kwenye eneo hilo la viraka kuna mtu anaitwa Lucho ambaye amefanikisha sana
kazi, lakini pia mshambuliaji yupo Paco Alcacer, aliyewafungia wana
Katalunya mabao mawili na usaidizi kwa mengine mawili katika dakika zake 376
alizocheza, zote akitokea benchi.
Yupo Denis
Suarez ambaye ni kiungo aliyefunga bao moja na usaidizi kwa mawili, ambapo
akiwa ni kiungo wa kati si kazi mbaya. Nimalizie kwa kusema kwamba kwenye
ulinzi wa kati Gerard Pique yupo vizuri sana lakini pia Marlon na huwezi kuacha
kumtaja mtu kama Javier Mascherano.
No comments:
Post a Comment