KLABU ya Yanga imeingia mkataba miaka mitano na kampuni ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa wenye thamani ya shilingi bilioni tano.
Mkataba huo unakuja siku tano baada ya watani wao Simba kusaini mkataba na kampuni hiyo wenye thamani ya bilioni 4.9 ambapo sasa klabu hizo zimepata neema ambazo zitazifanya kuendelea kufanya vizuri.
Mkataba huo utaifanya Yanga kupokea kiasi cha milioni 950 kwa mwaka wa kwanza kiasi ambacho kitakuwa kinaongezeka kwa asilimia tano kila mwaka.
Akizungumza na waandishi wa Habari baada ya kutiliana saini, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Clement Sanga alisema mkataba huo utakuwa msaada mkubwa katika uendeshaji kwa kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa ili kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika.
“Kuingia kwa SportPesa ndani ya klabu yetu kutakuwa na manufaa mkubwa kwani tumejadili masuala ya kuwa na uwanja, kuinua soka la vijana na mengi ambayo yataifanya Yanga kufanya vizuri kimataifa,” alisema Sanga.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa SportPesa Abbas Tarimba alisema dhamira yao ya kuwekeza katika soka la Tanzania ni kuziona timu za Simba na Yanga ambazo wameingia nazo mkataba zinafanya vizuri katika michuano mbalimbali.
“Leo tumeingia mkataba na timu nyingine ya Tanzania baada ya Simba ambayo tulimalizana wiki iliyopita sasa ni Yanga na msimu ujao itavaa jezi yenye nembo yetu kifuani,” alisema Tarimba.
Yanga itapata shilingi milioni 100 kama itafanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi msimu ujao kama ‘bonus’ ya mkataba huo.
No comments:
Post a Comment