MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji ametangaza kuachia ngazi rasmi
kuiongoza klabu hiyo, imefahamika.
Kwa mujibu wa Katiba, Yanga sasa itakuwa chini ya uongozi wa Makamu
mwenyekiti wake, Clement Sanga hadi pale uchaguzi wa kuziba nafasi hiyo
utakapofanyika.
Akielezea kujiuzulu kwa, Mani alisema kuwa ameamua kukaa pembeni ili
kuwapisha wengine nao waiongoza klabu hiyo.
"Nimeamua nipumzike nipishe wengine waongoze, Yanga ni yetu sote
nilipoingezewa muda tu kwa demokrasia, lakini haimanishi kuwa Mimi ndio nitakua
Mwenyekiti milele, " alisema Manji ambaye hata hivyo si mara yake ya
kwanza kutangaza kuachana na klabu hiyo.
Agosti mwaka jana pia alitangaza kujiuzulu ikiwa ni siku chache
tangu alipotangaza kutaka kuikodi timu hiyo kwa muda wa miaka 10, huku asilimia
75 za timu hiyo zikiingia kwake na kutoa asilimia 25 kwa timu hiyo kila mwaka
kitu kilichopingwa na wadau wengi wa Soka ikiwemo Serikali.
Hata hivyo, wanachama wa klabu hiyo walimpigia magoti na kumsihi
asitishe azma yake hiyo, ambayo alikubali kuendelea na uongozi hadi juzi
Jumamosi alipoijulisha rasmi kamati yake ya utendaji kuwa ni muda muafaka kwa
yeye kukaa pembeni.
"Nia yangu yakujiuzulu ni ya muda mrefu, sikutaka kufanya maamuzi
katikati ya ligi ningewachanganya wachezaji, nashukuru tumetetea ubingwa wetu
naiacha Yanga ikiwa na kikosi bora na hata makocha pia.
" Yapo mengi mazuri ninayojivunia Yanga ikiwemo umoja na
mshikamano, ikumbukwe nilingia wakati kuna mgogoro mkubwa, nikafanikiwa
kumaliza hivyo ni muda sahihi na muafaka kwa Mimi kukaa pembeni.
Ikumbukwe Yanga ni klabu ya wanachama, Yanga ni kubwa kuliko mtu
yoyote, naamini watakaofuatia wataendeleza pale nilipoishia, "
alisisitiza.
Kwa upande wa Katibu wa Yanga Charles Mkwasa akizungumzia hilo alisema
"Nimeona taarifa ya Mwenyekiti wetu kwenye mitandao, na nilikuwa
nawasiliana naye kila siku kwa email na hajawahi kunieleza hili, ila kama kweli
ni maamuzi yake basi tutayaheshimu," alisema.
Hatahivyo, kuondoka kwa Manji kunaweza kukawa si pigo sana kwa klabu
hiyo ya Jangwani ambayo tayari imesaini mamilioni ya fedha kwa kudhaminiwa na
Sports Pesa huku ikielezwa kuwa kuna makampuni kadhaa ambayo yapo mbioni
kudhamini timu hiyo ya mtaa wa Twinga na Jangwani.
No comments:
Post a Comment