Pages
▼
Tuesday, May 16, 2017
MAKUNDI, VITUO LIGI YA MABINGWA MKOA (RCL) 201718
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetangaza Makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL).
Kadhalika TFF, limetangaza timu saba kwa kila kundi katika michuano hiyo itakayoanza Mei 28, mwaka huu katika vituo vya Lindi, Songwe, Tabora na Kahama mkoani Shinyanga.
Ratiba mechi za kila kituo itatolewa Mei 22, mwaka huu.
Hata hivyo, michuano ya RCL imechelewa kuanza baada ya baadhi ya timu kushindwa kukamilisha vigezo vya ushiriki ikiwa ni pamoja na kulipia ada ya ushiriki kwa wakati, leseni za wachezaji kwa wakati pamoja na kuwasilisha usajili kwa wakati.
Mwisho wa kutimiza vigezo tajwa hapo juu ilikuwa Mei 15, 2017 lakini sasa TFF imesogeza mbele hadi Mei 18, mwaka huu ili timu ziweze kukamilisha taratibu za kulipa ada ya ushiriki na leseni za wachezaji.
Mwisho ilikuwa iwe Mei 15, 2017 lakini TFF kiungwana tu, imetoa tena siku tatu na hivyo mwisho za kukamilisha taratibu hizo itakuwa Mei 18, mwaka huu.
Tayari Makatibu wa Mikoa wamejulishwa hilo tangu Mei 5, mwaka huu, lakini sasa kwa timu ambazo hazitakamilisha taratibu za kulipia ada au leseni za wachezaji itaondolewa kwenye mashindano.
Kundi A litakuwa Mkoa wa Lindi ambako kutakuwa na timu za Shupavu FC ya Morogoro, Silabu FC ya Mtwara, Mbinga FC ya Ruvuma, Politan ya Dar es Salaam, Makambako Heroes ya Njombe, Ambassador ya Shinyanga na New Generation ya Mtwara.
Kundi B litakuwa Mkoa wa Songwe ambako timu za kituo hicho ni Kisarawe United ya Pwani, Moto Chini FC ya Mtwara, Makanyagio FC ya Katavi, Makumba ya Dar, Boma FC ya Mbeya, Real Mojamoja ya Iringa na Sahare All Stars ya Tanga.
Kundi C litakuwa Kituo cha Mkoa wa Tabora ambako kutakuwa na timu za Nyanza FC ya Manyara, Nyundo FC ya Kigoma, Eleven Stars ya Kagera, Bodaboda FC ya Arusha, Stand Misuna ya Singida, Majimaji Rangers ya Lindi na Area C United ya Dodoma.
Kwa upande wa Kundi D ambalo kituo chake ni Kahama mkoani Shinyanga, kutakuwa na timu za Dar City ya Dar, Buseresere ya Geita, Ndovu Sports ya Mwanza, Usamala FC ya Simiyu, Baruti FC ya Mara, Green FC ya Songwe na Msange FC ya Tabora.
No comments:
Post a Comment