MSHAMBULIAJI
wa Real Madrid, Karim Benzema amemgeuzia kibao mchezaji wa Lyon na timu ya Taifa ya Ufaransa,
Mathieu Valbuena, akidai alimwekea uongo juu ya tuhuma za kumhusisha na mkanda
wa video za ngono.
Benzema (29)
aliyekuja kutemwa kikosi cha Ufaransa, alidaiwa kuchonga mpango wa kupata kiasi
kikubwa cha fedha kutoka kwa Valbuena (32) anayechezea Lyon, akidai kuna
mshirika wake alikuwa na kanda za video za ngono za Valbuena na ikiwa hangetoa
fedha hizo, basi picha zingetundikwa mtandaoni na kumwaibisha.
Wakati suala
hilo likiendelea kwa utata kwa muda sasa huku ukweli ukiwa haujulikani, Benzema
ameibukia Madrid, Hispania na kudai kwamba rafiki yake huyo wa zamani ni mwongo
na mfitini aliyeamua kumharibia heshima yake mbele ya jamii na kwamba suala
lote hilo lilitungwa na Valbuena.
Benzema
akasema kwamba uongo wa Valbuena unamfanya achanganyikiwe kiakili, huku akibaki
nje ya kikosi cha timu ya taifa, akisema ni sawa na mtu aliyetupwa kwenye
matope.
Benzema
alidaiwa kutumia vipande vya kanda vilivyo kwenye simu ya mkononi kumtishia
Valbuena, akashitakiwa kwa usaliti.
Desemba
mwaka jana, korti iliyopo Versailles ilikataa maombi ya Benzema ya kutaka
kusitisha mwendelezo wa shauri hilo ambapo alishitakiwa kwa kula njama za
usaliti tangu Novemba 2015.
“Huyu jamaa
ana tatizo fulani …hii yote ni hadithi yake. Yaani ninapomsikia akisema eti
yupo tayari kucheza nami tena nashangaa, maana alshasema mie ni mchafu,
nilimtishia na kumtia hofu.
“Sasa
anasema eti asingefungua kesi kama angejua kwamba nilihusika. Kwa zaidi ya mwaka
mmoja unusu mie ndiye adui yake mkubwa zaidi, kijana mbaya, mhuni, natakiwa
kuadhiniwa, kutupwa kwenye matope, jina langu na la familia yamechafuliwa,”
anasema Benzema.
Mfaransa
huyo anasema kwamba hajamuona rafiki yake wa karibu, Karim Zenati, anayedaiwa
kuwa na kanda hizo, tangu kashfa hiyo iibuliwe, kwa sababu alizuiwa kumwona,
wakati ndiye ‘best’ wake na anasema yupo tayari kwenda jela kwa kosa ambalo
hakulifanya.
No comments:
Post a Comment