TIMU ya JKT Ruvu inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa
(JKT) imekuwa ya kwanza msimu huu kushuka daraja kutoka Ligi Kuu Tanzania Bara
baada ya leo kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Toto Africans.
JKT Ruvu imebakisha michezo miwili kabla ya kumaliza ligi
hiyo, ambapo hata kama itashinda yote itafikisha pointi 30 ambazo haziwezi
kuiokoa isishuke daraja.
Kwa mujibu wa kanuni za ligi hiyo msimu huu, timu tatu za
mwisho ndiyo zinashuka daraja, ambapo timu zilizo na pointi ambazo JKT Ruvu
inaweza kuzifikia ni Toto Africans yenye pointi 29 baada ya ushindi wa jana na
Majimaji ya Songea pia yenye pointi 29, baada ya jana nayo kuifunga Mwadui.
Timu inayoshika nafasi ya nne kutoka chini ni Ndanda FC
ya Mtwara yenye pointi 30, wakati African Lyon inashika nafasi ya tano kutoka
mkiani ikiwa na pointi 31 sawa na Prisons iliyopo nafasi ya 10 ikiwa na pointi
pia 31.
Kwa mazingira hayo baada ya JKT Ruvu kushuka daraja, hivi
sasa timu za Majimaji, Toto Africans, Ndanda FC, Lyon na Prisons zitakuwa
zikipambana kuepuka janga hilo na yoyote inaweza kuungana na JKT Ruvu.
Katika mchezo wa leo, JKT Ruvu ilikuwa ya kwanza kupata
bao dakika ya kwanza mfungaji akiwa Hassan Dilunga, kabla ya Toto kusawazisha
dakika ya 20 mfungaji akiwa Waziri Junior kwa kichwa kutokana na krosi ya
Mohammed Soud.
Dakika ya 35 Waziri Junior tena aliongeza bao la pili
baada ya kutumia vizuri pasi ya Mohammed Soud.
Katika michezo mingine jana, Mwadui ilikubali kipigo cha
mabao 3-0 kutoka kwa Majimaji ya Songea, huku Ruvu Shooting na Kagera Sugar
zikitoka sare ya bao 1-1.
No comments:
Post a Comment