PAZIA la
Ligi Kuu ya England (EPL) msimu wa 2016/17 linafungwa leo, ambapo ni timu mbili
tu zimeshajua kwa yakini kwamba zimefuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL)
lakini tatu za mkiani zimeshajihakikishia kushuka daraja.
Kila mmoja
amevuna kwa kadiri alivyopanda, bila shaka zikichanganywa humo bahati njema na
mbaya kwa wengine na ni wazi kuna watakaokuwa wakionesha au kuoneshewa vidole
kutokana na mienendo ya timu hadi ligi inamalizika.
Mabingwa ni
Chelsea wanajulikana na washindi wa pili ni Tottenham Hotspur – zote klabu za
hapa hapa jijini London, furaha iliyoje kwa wana wa jiji hili!
Kama kuna
kitu kinafuatiwa kwa makini Jumapili ya leo basi ni mechi tatu tu. Moja ni ya
Arsenal dhidi ya Everton, lakini wanaotazama huko watakuwa wakirusha macho
kwenye mechi baina ya Liverpool na Middlesbrough pale Anfield bila kusahau ile
ya Manchester City wanaokaribishwa Watford.
Upo
uwezekano wa kutokea Liverpool na Arsenal kuja kucheza mechi yao katika ligi
yap eke yao, ili kuchagua nani miongoni mwao asonge mbele. Jamaa hawa wanaweza
kukutana, lakini City ambao wanashika nafasi ya tatu wasidhani kwamba wapo
salama sana, japokuwa wanahitaji pointi moja tu.
Arsenal wana
pointi 72, moja pungufu ya Liverpool na tatu nyuma ya Man City. Arsenal
wanashika nafasi ya tano, Liverpool wa nne na City wa tatu. Kwa hiyo leo ni
vita ya timu hizi tatu kuwania kwenda kwenye mashindano makubwa zaidi Ulaya –
UCL. Timu moja itakosa, na italia, itatupwa ligi ndogo ya Ulaya – Europa
League.
Man City
wapo mbele kwenye mbio hizi za farasi watatu na wana nafasi kubwa ya kufuzu
moja kwa moja ikiwa watafanya kile washabiki wao wanachotaka leo hii wakati
Liver nao uwezekano wa kufuzu kwa nafasi ya nne upo mikononi mwao wakati
Arsenal ni ile ya fisi kusubiri mkono wa mwanadamu udondoke ndipo aule.
Ndio kusema
Arsenal hawana uamuzi na hatima yao, bali ni watu wa kupigana washinde, lakini
wakishashinda wategemee na matokeo ya watu wengine; licha ya jitihada zao
wanahitaji kusaidiwa na ama Middlesbrough au Watford kwa kuwafunga wapinzani
wao hao.
Kwa hali
ilivyo, kuna uwezekano kwamba leo haitakuwa siku ya mwisho ya msimu; ni kama
unaposema unaenda kuvunja kamati ya sherehe fulani lakini ikakwama kuvunjika
kwa sababu fulani.
EPL nayo
inaweza isimalizike leo na makocha Pep Guardiola, Jurgen Klopp na Arsene Wenger
wakaachwa wakitowelea juu ya hatima ya muhula wao kwa muda zaidi kidogo,
ikitokea yoyote kati ya timu zao inamaliza ligi ikiwa na rekodi zinazofanana na
mahasimu wao.
Hiyo
itatokea iwapo timu husika zinafungana kwa pointi, mabao ya kufunga nay ale ya
kufungwa. Ikitokea hivyo kwa Arsenal na Liver itamaanisha kwamba timu hizo
zitakutana kwa mara ya tatu msimu huu badala ya mbili za kawaida na wakitoshana
nguvu basi penati kwa ajili ya kuamua.
Hapana
ubishi kwamba Arsenal wanakabiliwa na mtihani mgumu zaidi – kucheza dhidi ya
Everton, hata kama ni Emirates. Hawa ndio walianza kuwatibulia msimu kwa
kuwafunga Arsenal kule Goodison Park. Itakuwaje basi ili timu hizi zikutane kwenye
mechi ya ziada ya mtoano? Nifuatilie:-
1.
Arsenal v Liverpool (kuwania nafasi ya nne)
Arsenal na
Liverpool wanaweza kuja kukwaana na Liverpool iwapo watamaliza kwa idadi sawa
ya rekodi kama nilivyotaja hapo juu. Itakuwa hivyo ikiwa Liverpool watafungwa
2-0 na Middlesbrough huku Arsenal wakienda sare ya 1-1 na Everton. Pia
watamaliza wakiwa na rekodi sawa ikiwa Liverpool watafungwa 3-1 na Arsenal
kwenda sare ya 2-2 na Everton. Ngoma inogile.
2. Liverpool v Manchester City
(kuwania nafasi ya tatu)
Liverpool na
Manchester City watamaliza wakiwa sawa kwa takwimu iwapo Man City watakwenda
sare ya 3-3 huku Liverpool wakiwafunga Middlesbrough 3-0. Pia watatoshana nguvu
ikiwa City wataenda sare ya 4-4 huko Vicarage Road huku Liverpool wakishinda mechi
yao kwa mabao 4-1, na kadhalika.
3. Arsenal v Manchester City (kuwania
nafasi ya nne)
Arsenal na
Manchester City watamaliza wakiwa na rekodi za kufanana iwapo Arsenal
watawafunga Everton 1-0, Manchester City wapoteze 4-0 kwa Watford na Liverpool wawafunge
Middlesbrough. Pia watamaliza wakiwa na alama zote sawa iwapo Arsenal
wanashinda 2-1 na City kufungwa 5-1, na mikokotoo mingine ya namba kwa tofauti
ya mabao kama hivyo.
Kwa msingi
wa niliyoyaweka hapo juu, ni kwamba kila moja kati ya klabu hizi tatu
inakabiliwa na uwezekano wa kumaliza kwa idadi sawa na mwenzake na hivyo
kutakiwa kujiandaa kwenda kwenye uwanja huria kucheza kujipanga upya, hali hiyo
ikionekana kunukia zaidi kwa Liverpool na Arsenal.
Je, hii
itakuwa moja ya zile siku ambazo The Reds, yaani Liverpool hujikwaa bila
kutarajiwa? Je, Wenger atafanikiwa kuendeleza mserereko wa kuwa ndani ya UCL
mfululizo au ndio mwisho mchungu? Kujiamini kwa Guardiola kunamaanisha anavuka
au bado anaweza kuwa nje ya UCL? Ameshaweka rekodi mbaya ya kukosa kikombe
chochote kwa mara ya kwanza tangu aanze ukocha.
No comments:
Post a Comment