*Mourinho
kujenga heshima baada ya kupigwa 4-0?
*Conte
anataka kuonesha hakubahatisha hapo awali
LEO
kuna mambo makubwa, wakati Wakristo wakiadhimisha ibada ya Pasaka na sherehe
zake, kwenye soka kuna mechi kubwa baina ya vinara wa ligi, Chelsea
wanaokaribishwa na Manchester United.
Chelsea
wamefunga safari kwa ajili ya mechi hii wakiwa wanajiamini zaidi, lakini pia
wakifurahia uendelevu wa kuwapo kwao kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu ya England
(EPL) kwa idadi kubwa ya pointi, United wakiwa nafasi ya tano.
Wakati
Chelsea wamejikusanyia pointi 75 katika mechi 31, United ambao wamekithiri kwa
sare wanazo pointi 54. Chelsea wanafurahi kuwakabilia Man U wikiendi hii, kwani
wametulia kwa siku nane bila kucheza mechi.
Tofauti
kabisa, wapinzani wao, Manchester United wanaingia uwanjani baada ya safari ya
Ubelgiji walikotoka kucheza na Anderlecht katika mechi za Ligi ya Europa
Alhamisi iliyopita dhidi ya Anderlecht ya hukomchezo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1jambo ambalo hapana shaka limewaongezea uchovu.
Antonio
Conte anatambia mwenendo wa kuridisha wa Chelsea hadi sasa katika msimu wake wa
kwanza hapa England wakati Jose Mourinho bado anaendelea kukisuka kikosi chake,
kwa kuangalia nani akae wapi.
Old Trafford
inatapika leo kwa ajili ya watu kushuhudia mechi hii kubwa, wakiwa ni washabiki
wa United wenyeji lakini pia wale wa Chelsea walio Manchester na wengi zaidi
wanaosafiri kuwaunga mkono vijana wao.
Timu mbili
hizi zinapokutana huwa kuna mengi ya kuvutia, iwe ni mwanzoni mwa msimu au hata
mwishoni kama sasa, bila kujali ni timu ipi bingwa, iliyo mbele ya mwenzake
kwenye msimamo wa ligi au wanapishana vipi.
Huwa ni
wakati wa kulinda heshima, kila mmoja akitaka mwingine amheshimu. Ni sahihi kusema
kwamba mechi baina ya fahali hawa wawili ni moja kati ya zinazokuwa moto zaidi
na kwa kawaida washabiki huwasha fashifashi.
Hata hivyo,
haikuwa hivi tangu zamani, kwa sababu uhasama baina ya klabu mbili hizi si wa
jadi bali umekuja katika zama hizi. Uhasama wa jadi ni baina ya Manchester
United na Liverpool na huo ni kitaifa, wakati Chelsea mahasimu wao ni Arsenal,
na hao ni wa jijini London.
Uhasama
kwenye soka hapa nchini, pamoja na mambo mengine, umetokana na mambo kadhaa,
yakiwamo eneo la jiografia klabu zinapotoka au ushindani uliozidi sana kwa
ajili ya kuwania heshima baina ya klabu mbili husika.
Wanaocheza
leo wapo mbalimbali sana, wanatenganishwa na umbali wa maili 170, njiani humo,
au kwenye mizingo, kukiwa na klabu nyingine nyingi tu, zikitenganisha fahali
hawa wawili. Ni kwa msingi huo, nasema kwamba huu ni ushindani wa kuwania
heshima na si ule wa eneo la kijiografia.
Klabu zote
mbili wamepata kufurahia mafanikio kabla ya zama hizi, kwenye miaka ya ’50 na
mwishoni mwa ’60, wakati United ya zama za Matt Busby – lakini zama za sasa
hazingeweza kuwekewa uendelevu mrefu wa kutosha kwazo kushinda ilhali uhasimu
kwa asili haukupata kuundwa.
Baada ya
tasa ya miaka 26, Manchester United, chini ya Alex Ferguson walitwaa ubingwa
wao kwa mara ya kwanza 1993 na tangu hapo ukaanza ujenzi wa kile kilichoitwa
moja ya ngome imara za soka katika historia ya England.
United
walipata kuja kuingia kwenye uhasimu fulani ulioburudisha sana dhidi ya
Newcastle, lakini ulichukua muda mfupi kabla ya Arsenal kuwapandia na kutaka
kuwapokonya chakula kwenye sahani na kuwa wapinzani wakubwa na tishio ka Fergie
mwishoni mwa miaka ya ’90 na mapema miaka ya 2000.
Baadhi ya
vita ambazo klabu mbili hizi zimepigana zitabaki kwenye kumbukumbu ya muda
mrefu. Kuwasili kwa bilionea wa Urusi, Roman Abramovic Stamford Bridge na
kuonwa kama mifuko yake haioni mwisho 2003 kulionesha mwanzo wa ushindani
mkubwa baina ya klabu hizi.
Kwa nini?
Ieleweke kwamba United ni moja ya klabu kubwa hapa England lakini hata Ulaya,
hivyo walikuwa wakitamba sana England, sasa kuibuka kwa bilionea ambaye
anamwaga fedha, anasajili wachezaji wakubwa, hachukui gawio mwaka wa fedha
ukikamilika kunawatisha wapinzani.
Manchester
wakaona kwamba mambo si rahisi tena, hali si lele mama bali lazima kujituma
hasa ndani na nje ya uwanja. Abramovich akamleta Jose Mourinho London, na baada
ya kuwa bila ubingwa tangu 1955, Chelsea (mpya sasa) wakatwaa ubingwa wa
England.
Mourinho ni
wa kushukuriwa kwa jinsi alivyowajenga Chelsea wakawa walivyo kabla ya
kuondoka, akarejea mara ya pili, akaboronga na kufukuzwa kisha akajiunga upande
wa pili – Manchester United, na leo wanacheza, ikiwa ni mechi yake ya pili
akiwa huko.
Ile ya awali
msimu huu, ilifayika Oktoba 23, siku ya Jumapili kama leo, na Mourinho
aliondoka huko kwa aibu kubwa, kwani Conte hakumwonea huruma, akiwaacha vijana
wake kuwasasambua Mashetani Wekundu 4-0.
Mreno
huyu (Mourinho) alitumia vyema fedha za bosi wake kutwaa ubingwa mara mbili,
Kombe la FA na makombe mawili ya Ligi katika kipindi cha miaka mitatu iliyokuwa
kama ya upepo wa kinyamkera jijini London.
Wakati klabu
mbili hizo zilikuwa zikipigania heshima dimbani, nje ya uwanja Fergie alikuwa
akifurahia vijembe vyake dhidi ya makocha wengine, na ilifika mahali Mourinho
akadai kwamba Fergie hakuwa na heshima isipokuwa kwake mwenyewe.
Kupigana
kwao vijembe na kutunishiana misuli kuliambukizwa kwa wachezaji wao pia, ambapo
kwenye mechi kulikuwa na undava pia, lakini kila upande ukitaka uibuke na
ushindi.
Mourinho
alipoondoka kwenda kuwafundisha Real Madrid, Ferguson alisema ‘Ligi Kuu
imempoteza kijana mwenye bunduki aliyekuja mjini akitaka kupambana na mzee
mlinda Amani.”
Wawili hao
walikuja kuonekana wakijenga urafiki, ikadhaniwa Mourinho alikuwa akivizia
kupewa kazi baada ya Fergie kustaafu, lakini hakupewa, badala yake akapewa
Mskochi mwenza na Fergie, David Moyes, aliyefukuzwa miezi 10 tu baadaye.
Hata hivyo,
aliipata kazi hiyo baada ya kocha mwingine, Louis van Gaal kushindwa misimu
yake miwili na kutimuliwa, wakati Mourinho naye akiwa hana kibarua baada ya
kufukuzwa Chelsea alikofanya vibaya kiasi cha kuielekeza timu kwenye kushuka
daraja.
Leo sasa
katika mechi ya pili dhidi ya timu yake ya zamani aliyosema aliipenda sana,
Mourinho anataka kuwaonesha kwamba yeye ni zaidi, lakini pia alipe kisasi cha
kufungwa 4-0 mechi ya kwanza, jambo ambalo linaonekana zito kiasi, lakini
kwenye soka wanasema mpira unadunda, hivyo lolote linaweza kutokea.
Kwenye bodi
za wakurugenzi kumebadilika, ambapo Peter Kenyon yeye aliondoka United kwenda
Chelsea, akisema kwamba waajiri wake wapya wangekuwa klabu kubwa zaidi duniani
ikifika 2016; bado hawajawa, mwaka mmoja baadaye.
Fergie
alichukia kuondoka kwa Kenyon, akisema iweje aende kwenye klabu isiyokuwa na
historia ya kabla.
Washabiki wa
United wanasema kwamba kwao, mahasimu wanaotangulia ni Liverpool, Manchester
City, Leeds United kisha ndio matajiri hao wa London. Chelsea wao wanasema
wanaanza na Arsenal kisha Tottenham Hotspur.
Historia ya
karibuni ya timu hizi mbili inaonesha kuwa wachovu kiasi, kushindwa kufuzu kwa
Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), lakini Chelsea wanaonekana kurudi huko mwaka huu,
wakati United wanatakiwa kukaza msuli ili kuwapiga kumbo Man City na Arsenal
washike nafasi ya nne.
No comments:
Post a Comment