*Pointi
zinazopokwa si lazima wapinzani wapewe
USHINDI
wa timu upo mara mbili – uwanjani na mezani; hii si kwa Tanzania tu bali hata
huko duniani, ambapo ushindi wa uwanjani huweza kutenguliwa, mshindwa akapewa
mshindi na mshindi akapewa unyonge.
Ndivyo
ilitokea juzi kati hapa, ambapo Simba walipewa pointi tatu dhidi ya Kagera
Sugar, kutokana na timu hii ya pili kuchezesha mchezaji ambaye hakuwa na sifa.
Kwenye mechi
hiyo muhimu kwa Simba kuwania ubingwa, walifungwa na Kagera 2-1 na hivyo kuwapa
wapinzani wao wa jadi – Yanga, mwanya wa kuwapiku kwa kutetea tena taji hilo.
Hata hivyo, Simba walikwenda kukata rufaa, wakidai mchezaji Mohamed Fakhi
alikuwa na kadi tatu za njano.
Kamati ya
saa 72 ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) wamewapa Simba ushindi wa mabao
2-0 na pointi tatu hivyo kuwapaisha hadi pointi 61 katika nafasi yao ya kwanza,
huku Yanga wakiwa nazo 56 na mchezo mkononi.
Simba jana
ilicheza mechi nyingine ya ligi hiyo na Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba,
Mwanza, hivyo makala haya yameandaliwa kabla ya mchezo huo.
Visa vya
jinsi hii vya ushindi wa mezani, ambao watu wengi huupinga na kusema bora mechi
kurejewa, vimepata kujitokeza Tanzania, lakini pia kwenye sehemu nyingine
katika ngazi ya klabu na pia ya timu za taifa.
Kwa Tanzania
matukio kama haya yamepata kutokea, siku za mbele nitawaeleza katika makala
nyingine, lakini kwa leo ngoja nizungumzie katika nchi zilizoendelea.
Matukio ya
aina hii kwa nchi zilizoendelea kisoka ni machache, kwani kumbukumbu huwekwa
vyema na wadau, ikiwa ni pamoja na kocha, mchezaji mwenyewe, na benchi la
ufundi kwa ujumla.
Lakini pia
chama cha soka huziweka na huweza kukumbushia klabu ili kuepuka fadhaa. Kuna
sehemu nyingine watu huviziana tu, akicheza, hola! Ushindi wa mezani.
Kwa mfano
kwneye Ligi Kuu za England, Hispania, Ufaransa, Italia, Ujerumani na kwingineko
si rahisi kusikia mambo kama hayo.
Mchezaji
kukosa sifa huwa ni kwa sababu mbalimbali, na si kuwa na kadi kadhaa za njano
au moja nyekundu.
Mchezaji
hukosa sifa ikiwa taratibu za usajili zilikiukwa, alishachezea timu mama
(tuseme timu A) kwenye mashindano husika kabla ya kupelekwa kwa mkopo timu B.
hata hivyo, imetokea katika EPL timu kuadhibiwa kwa kuchezesha wachezaji
waliokosa sifa.
Kwa kawaida
makocha ndio huingia kwenye aibu kwa kosa kama hilo. Hata hivyo, kupokwa pointi
timu moja si lazima nyingine ipewe, na hii ilitokea 2010 baada ya mechi ambayo
Brighton walifungwa 2-0 to Hartlepool United.
Kocha wa
Brighton, Gus Poyet, alisonga mbele na kuandaa rufaa ili wapinzani wao wapokwe
pointi na kuadhibiwa kwa sababu walichezesha mchezaji aliyekuwa na kadi, Gary
Liddle.
Chama cha
soka kweli kikafanya uchunguzi na kubaini mchezai huyo alikuwa amezuiwa kucheza,
kikawapokonya Hartelepool pointi tatu na mabao mawili na kuwapiga faini ya
pauni 3,500.
Hata hivyo,
Poyet na Brighton waliachwa wamekasirika, kwa sababu hawakupewa pointi hizo,
badala yake zilipelekwa kwa chama cha soka. Poyet alionesha hisia zake na kusema
walikosea kabisa.
Mwaka 2014,
timu ya Alfrteton Town walio Conference Premier ya England nao walipokonywa
pointi tatu kwa kuchezesha mchezaji ambaye hakuwa na sifa wakapata ushindi wa
3-1 dhidi ya Kidderminster.
Golikipa Jon
Worsnop, aliyekuwa amesajiliwa kwa mkopo wa dharyra kutoka FC United ya
Manchester alicheza kwenye mechi hiyo, na kilichogomba ni kwamba hadi anacheza,
bado kwenye mtandao usajili wake haukuwa umekamilika, hivyo watu wakaona na
uamuzi kuchukuliwa.
Adhabu hiyo
ni sawa na iliyokuwa imetolewa dhidi ya Oxford City na Harrogate Town,
waliokiuka pia kanuni za ligi msimu huo.
Tukichambua
zaidi tunawakuta jamaa wanaoitwa Rob Purdie na Jake Robinson wa Hereford United
na Torquay Town wa England, ambapo katika mazingira yasiyo ya kawaida, timu
zote zilichezesha wachezaji wasio na sifa.
Mechi
ilimalizika kwa ushindi wa 3-1 kwa Hereford ambayo ilishuhudia kiungo Purdie na
mshambuliaji Robinson wakicheza licha ya kwamba hawakuwa wamesajiliwa rasmi
kwani dirisha la usajili la Januari lilitokea kufungwa kabla ya wao kuwa ndani,
hivyo wakabaki nje.
Kila klabu
ilimshitaki mwenzake kwa kukiuka kanuni za ligi, laiti wangekaa kimya, maana
wote walilimwa faini ya pauni 17,500, kisha mshindi akapokwa pointi tatu na
mshindwa pointi moja – faida kwa chama cha soka, kilichopata fedha na pointi
zikarejeshwa kwenye shubaka.
WACHEZAJI SITA WA
FC SION
Pengine
kitu cha kutazama kwa mshangao ni kitendo cha timu ya Uswisi ya Fc Sion
kuchezesha wachezaji sita wasio na sifa, nayo ilikuwa 2011. Adhabu yake ilikuwa
kali sana, kwani walipokonywa pointi tatu kwa kila mchezaji batili, ikimaanisha
walinyang’anywa pointi 36.
Yaani ukali
wa adhabu ulimaanisha kwamba wamebaki na pointi hasi, maana hawakuwa nazo hata
hizo walizonyang’anywa, na wakatupwa nje ya michuano ya Ulaya. Klabu hiyo
wakati huo walikuwa chini ya marufuku ya usajili iliyowekwa na Shirikisho la
Soka la Kimataifa (Fifa).
Hata hivyo,
kwa kichwa ngumu, walisonga mbele na kusajili wachezaji sita kisha wakawatumia
kwenye mechi ya Ligi ya Europa dhidi ya Celtic wa Uskochi.
Awali Chama
cha Soka (FA) cha Uswisi kilisita kuadhibu klabu hiyo had Fifa walipotishia
kupiga marufuku timu ya taifa na klabu nyingine kushiriki michuano ya
kimataifa.
Barani
Afrika kuna kumbukumbu ya Guinea ya Ikweta kupokwa pointi tatu kutokana na
kuchezesha mchezaji asiyekuwa na sifa kwenye mechi ya kufuzu kwa fainali za
Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Cape Verde.
Ajabu ni
kwamba mchezaji mwenyewe anachezea klabu kubwa kiasi ya Hispania, Mallorca,
naye ni Emolio Nsue Lopez, aliyecheza kwenye ushindi wa 4-3 Guinea ya Ikweta walioupata
dhidi ya Cape Verde. Cape Verde walipewa ushindi na washindi wakapokwa.
‘Sinema’
haikuishia hapo, kwani Cape Verde nao waliishia kutupwa nje ya mashindano baada
ya kuja kubainika kwamba nao walikuwa na mchezaji asiye na sifa ambaye
alicheza. Walisikitika sana kwa sababu walishinda mechi mechi ya kuamua nani
asonge mbele dhidi ya timu ngumu ya Tunisia.
No comments:
Post a Comment